Waliofaulu mtihani wa marudio watakiwa shuleni
OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa kushirikiana na Kamati za Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika mikoa husika, imekamilisha kuwapangia shule wanafunzi wote 2,096 waliofaulu mtihani wa marudio katika shule mbalimbali za sekondari.
Katibu Mkuu Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe amesema hayo Januari 15, 2023 mjini Morogoro, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa marudio Desemba 21/22 mwaka 2022.
Amesema baada ya kukamilika kwa maandalizi hayo, wanawataka wanafunzi waliofaulu kuripoti katika Shule walizopangiwa kuanzia Janauri 16, mwaka huu, ili kuanza masomo na wenzao.
Amesema Tamisemi ilipokea matokeo ya mtihani huo, ambapo jumla ya wanafunzi 2,096 wakiwemo wavulana 1,073 na wasichana 1,023 sawa na asilimia 96.15 ya watahiniwa waliofanya mtihani wamepata sifa ya kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.