Waliofungwa kwa unyanyasaji wa kingono wanaweza kukata rufaa

KATIKA uamuzi wa kihistoria, Jaji wa Kenya ameruhusu watu waliopatikana na hatia na kufungwa kwa unyanyasaji wa kingono kama vile unajisi, ulawiti na ubakaji kuwa huru kuwasilisha rufaa katika Mahakama Kuu ili kupitiwa tena kwa hukumu zao.

Unajisi unaweza kujumuisha vitendo vya ngono na mtoto au mtu mzima pia mwanamume kufanya mapenzi na mtu mwenye uhusiano naye wa damu kama vile ndugu na jamaa wa karibu katika familia.

Jaji wa Mahakama ya Juu, John Mativo alisema kuwa baadhi ya miongozo ya hukumu iliyokuwa ikitolewa ilikuwa ya kibaguzi hivyo kuhitaji kupitiwa upya na kurekebishwa ili ziendane na wakati uliopo.

“Adhabu za chini za lazima zinakiuka haki za mshtakiwa chini ya Kifungu cha 27 cha Katiba,” ulisema sehemu ya uamuzi huo baada ya kutolewa katika mahakama moja mjini Nairobi na kupokewa kwa shangwe na wanaharakati wa Haki za Binadamu.

Mwongozo wa hukumu hiyo unasema kwamba wafungwa wote wa unajisi wanapaswa kufungwa kifungo kisichopungua miaka 11.

Uamuzi huo unatokana na ombi kwa mahakama ambalo lilidai kuwa kifungo cha chini cha lazima kinachotolewa chini ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana kinakandamiza kupatikana kwa hukumu ya haki iliyohakikishwa chini ya Kifungu cha 50 cha Katiba ya Kenya.

Kifungu cha 50 kinasema kila mtu ana haki ya kulalamika chochote ambacho anaamini kinaweza kutatuliwa kupitia matumizi ya sheria.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button