UKAME na njaa inayoendelea kuutikisa Mkoa wa Arusha na baadhi ya maeneo nchini umewafanya wananchi waliokataa kuhama kwa hiyari kutoka Bonde la Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kujutia hatua hiyo, kutokana na mifugo kufa kwa njaa kila siku.
Viongozi wa wilaya za Ngorongoro na Handeni waliliambia HabariLEO jana kuwa maisha ya wananchi katika bonde la Ngorongoro kwa sasa ni ya mateso makubwa ikilinganishwa na Msomera kutokana na mvua zilizoanza kunyesha katika Wilaya ya Handeni na kuleta ahueni kwa wafugaji.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala alisema kutokana na ukame wa muda mrefu, idadi ya mifugo inayokufa wilayani humo imeongezeka na kuwa kubwa ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, maeneo ambayo kipindi cha nyuma yalikuwa na maji mengi huko Ngorongoro yamekauka mapema na kusababisha shida kubwa ya maji ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Aliongeza kuwa suluhisho la wafugaji wa Ngorongoro ni kwenda katika maeneo yenye miundombinu imara ya malisho na maji iliyojengwa na serikali Msomera wilayani Handeni.
“Unajua mifugo inakufa sana ikilinganishwa na wanyamapori kwa sababu wanyamapori wana maji ya kutosha kule kwenye kreta, hivyo wanaweza kusafiri kwa safari ndefu wakapata maji ya kutosha lakini wafugaji hawawezi kwenda kwenye kreta kwa ajili ya maji,” alisema.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni, Mashaka Mgeta alisema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo ya malisho kwa wafugaji wa Msomera na Handeni kwa ujumla yameongezeka na kufanya wafugaji kusahau kupoteza mifugo yao kutokana na ukosefu wa malisho na maji.
Alisema wakazi wa Msomera wanafurahia juhudi za serikali za kuwatafutia vyanzo mbalimbali vya maji na kufanya hali ya upatikanaji wa maji kwa wafugaji na wakulima kuwa nzuri.
Alisema kwa kujua athari za kubadilisha mazingira serikali iliandaa mazingira ya kupambana na changamoto za kubadili mazingira kwa kujenga majosho saba ya kuogesha mifugo pamoja na kujenga zahanati ya kutoa huduma kwa wananchi wa Msomera.
Aliongeza kuwa huduma za usafiri zimeimarika kwa kuanzisha usafiri wa magari kutoka Msomera kwenda Handeni Mjini ambapo kwa sasa nauli iimeshuka baada ya kuanzisha usafiri wa magari kutoka Sh 15,000 – 25,000 kwa pikipiki hadi kufika Sh 5,000 -7,000 kwa gari.
“Sasa hivi katika Kijiji cha Msomera kuna kiwanda cha kutengeneza mikate hali iliyoleta unafuu mkubwa wa maisha kwa wakazi wake, hivyo hata hao ambao hawajahamia huku tunawahakikishia kuwa huduma zote za kibinadamu zipo,” alisema Mgeta.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Msomera Kata Misima, Martin Oleikayo Paraketi aliishukuru serikali kwa kuwajengea wafugaji na wakulima miundombinu rafiki hususani miundombinu ya maji na kuwajengea majosho kwa ajili ya mifugo.
Aliwataka wananchi waliokataa kuja Msomera kubadili mawazo yao kwa kuwa wakiwa Ngorongoro wanakosa mahali mbadala pa kupeleka mifugo yao lakini wakiwa Msomera kuna sehemu mbalimbali za kupeleka mifugo yao ikiwa kutatokea ukame.
Aliiomba serikali kuangalia utaratibu utakaofaa kuwasaidia wananchi wa Msomera kupata chakula kwa bei nafuu kwani kwa sasa gunia moja linauzwa kwa gharama ya Sh 150,000 hali inayokuwa ngumu kwa wananchi wa hali ya chini.