SERIKALI imefafanua kuwa Wananchi wa Ngorongoro wanaohamishwa kutoka eneo la hifadhi kwenda kijiji cha Msomera Handeni Mkoa wa Tanga wamehamishwa kwa kuzingatia haki za binadamu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda amesema hayo Disemba 4 mkoani Morogoro wakati akifungua kongamano la siku mbili kujadili masuala ya ardhi.
Amelitaka Jukwaa la Ardhi Tanzania (TALA) na wadau wa mkutano huo kwenda kijiji cha Msomera na watakapotoka huko serikali iko tayari kupokea maoni.
Kongamano hilo la siku mbili lililobeba kauli mbiu ya Usalama wa Milki za Ardhi kwa Uhakika wa Chakula limejadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya ardhi ikiwemo haki za wanawake katika muktadha wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na usalama wa chakula, mipango ya matumizi ya ardhi na uratibu wa takwimu pamoja na hali ya haki za ardhi kwa vijana na utekelezaji ya mikakati na uhamasishaji vijana Kushiriki katika Kilimo.