DODOMA: SERIKALI imesema zaidi ya Sh Bilioni 7 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa Kijiji cha Ngombo Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliaisili na Utalii, Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la Antipas Mgungusi aliyetaka kujua serikali itaanza lini kulipa fidia wananchi wa Kijiji cha Ngombo waliopisha Hifadhi ya Pori Tengefu la Kilombero.
Soma pia: https://habarileo.co.tz/wananchi-ngara-kulipwa-fidia-sh-bilioni-26/
Kitandula amesema kuwa Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri 8 ilielekeza Kijiji cha Ngombo kufutwa na wananchi wake kuhamishiwa maeneo mengine sambamba na eneo la Pori Tengefu Kilombero kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba.
Soma pia: https://www.instagram.com/habarileo_tz/p/C50cWNMNNs8/?img_index=1
Amesema kuwa uwepo wa Kijiji cha Ngombo pamoja na vijiji vingine ndani ya pori hilo ulifanya ukubwa wa eneo la pori kupungua kwa asilimia 61.5 kutoka kilometa za mraba 6,500 hadi kilometa za mraba 2,500.
Katika hatua nyingine, waziri Kitandula akijibu swali la Mbunge Josephine Genzabuke ametoa wito kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki kwa wahifadhi wote kuruhusu wananchi ambao wamelima mazao kwenye maeneo yaliyohifadhiwa wavune mazao hayo, lakini wasiruhusiwe kulima tena kwenye hifadhi.