Walioiba fedha Z’bar kukiona, ZAEC kufumuliwa

Mwalimu auawa na mpenzi, kisa milioni 13/- za mkopo

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema watendaji wote wa serikali waliotajwa kwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar na kuhusishwa na upotevu fedha watachukuliwa hatua za kisheria.

Katika kujenga ufanisi wa Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA) katika utekelezaji wa majukumu yake, ameahidi kuijenga upya na kufanya uteuzi wa mtendaji wake hivi karibuni.

Dk Mwinyi alisema hayo Ikulu Jumatatu wakati alipofanya mazungumzo na wahariri na waandishi wa habari katika mkutano wa kawaida wa kila mwezi.

Advertisement

Alisema ZAECA imekabidhiwa majukumu makubwa kwa mujibu wa sheria, lakini kwa bahati mbaya haijatekeleza wajibu wake ikiwamo kuwachukulia hatua watu waliohusika na upotevu wa fedha kwa mujibu wa ripoti ya CAG.

Alisema anakusudia kujenga taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zenye uwezo na majukumu ya kupambana na rushwa kwa lengo la kukomesha maovu hayo.

“Tutaijenga (ZAECA) upya ikiwemo mifumo yake kuona inakuwa endelevu ambapo naahidi fedha zote za serikali zilizopotea tunahakikisha zitarejeshwa na watu waliohusika watawajibika,” alisema Dk Mwinyi.

Aidha, alitoa maelekezo na kuzitaka taasisi zinazohusiana na mwenendo wa kesi ikiwamo Mkurugenzi wa Mashtaka na Makosa ya Jinai (DPP) kufuatilia na kupeleka kesi hizo mahakamani.

Alizitaka mahakama kuhakikisha kesi zinazohusika na tuhuma za rushwa na uhujumu wa uchumi zinaendeshwa kwa haraka.

Alisema tayari ameagiza kila hoja za ripoti ya CAG kuchukuliwa hatua zaidi ikiwamo waliohusika.

“Hayo ndiyo maelekezo yangu kwa taasisi zinazosimamia mwenendo wa kesi na matukio ya hujuma kuhakikisha kesi zinaendeshwa kwa haraka na wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Dk Mwinyi.

Alibainisha kuwa hivi karibuni anatarajia kumteua Mtendaji Mkuu wa ZAECA ambaye miongoni mwa majukumu yake makubwa ni kumkabidhi ripoti ya CAG kwa ajili ya kuifanyia kazi. Aliyekuwapo alijiuzulu hivi karibuni baada ya ofisi yake kunyooshewa kidole na Rais.

Dk Mwinyi alisisitiza watendaji wote waliohusika na matukio ya upotevu wa fedha watafikishwa mahakamani na kusisita haitojali kwamba watendaji hao wanatokana katika awamu gani ya SMZ.

Alimpongeza aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ZAECA, Ahmed Khamis Makarani kwa kujiuzulu wadhifa wake kwa sababu amekabidhi wa majukumu makubwa ya kufuatilia masuala ya rushwa.

“Hivi karibuni nitamteua Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu wa Uchumi ambaye nitamkabidhi ripoti kwa ajili ya kufuatilia tuhuma zote na wahusika kufikishwa mahakamani. Nawahakikishieni watendaji waliohusika watawajibika bila ya kujali wanatoka katika awamu gani ya uongozi,” alieleza.

Dk Mwinyi aliwataka wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini, kufuata maelekezo na masharti ya uwekezaji ili kuepuka utapeli unaojitokeza.

Alisema sheria za uwekezaji zipo wazi ambazo mwekezaji mwenye nia ya kuwekeza anatakiwa kwenda Mamlaka Huru ya Vitega Uchumi na Uwekezaji (ZIPA) ambako atapata mwongozo na masharti ya kuwekeza.

Dk Mwinyi alisema hayo baada ya kuulizwa kuhusu muwekezaji aliyekuja nchini na kuonesha nia ya kuwekeza, lakini inadaiwa alitapeliwa eneo la ardhi na kufungua kesi mahakamani ambayo imekuwa ikisuasua.

“Jamani hata ninyi waandishi wa habari hebu waelimisheni wawekezaji wetu…tunao utaratibu unaofahamika kwa mujibu wa sheria ambapo Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi (ZIPA) ndiyo inayohusika na mambo hayo ambapo lengo ni na kuondosha urasimu uliokuwepo awali,” alisema Dk Mwinyi.

 

 

 

Kamati ya Bunge yapongeza maono ya EAC

Na Mwandishi Maalumu

 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeipongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kutafsiri kwa vitendo maono yake.

 

Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Vita Kawawa walisema hayo wakati wa ziara kutembelea miradi ya kikanda ya barabara ya EAC katika mikoa ya Dodoma, Manyara na Arusha.

 

Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilieleza kuwa ziara hiyo iliratibiwa na wizara hiyo na kutoa fursa kwa kamati kuona baadhi ya miradi ya EAC.

 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ziara hiyo pia ililenga kuonesha namna Tanzania inavyoshirikiana na Sekretarieti ya EAC na nchi wanachama kutekeleza miradi hiyo, kuanzia kufanya uchambuzi yakinifu na baadaye kutafuta fedha za utekelezaji.

 

Wajumbe walielezwa kuwa Tanzania imepakana na nchi tano za EAC; Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na katika nchi zote hizo kuna miradi ya barabara ya kuiunganisha Tanzania na nchi hizo.

 

Miradi michache ambayo ipo katika ujenzi ni barabara ya kutoka Kabingo, Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilometa 260 inayounganisha Tanzania na Burundi.

Barabara ya kutoka Tanga, Pangani, Saadani hadi Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 256 inayounganisha Tanzania na Kenya. Ujenzi wa barabara hiyo utajumuisha pia daraja la Pangani la mita 500.

 

Kwa upande wa Tanzania na Uganda, kuna mradi wa barabara ya Mutukula, Kyaka, Kasulu hadi Benaco yenye urefu wa kilometa 124 na Bugene, Burigi, Chato hadi Kasulo yenye urefu wa kilometa 68.

 

Wakikagua barabara ya kikanda ya Arusha, Namanga, Athi River na Barabara ya Mzunguko ya Arusha, wajumbe walieleza namna ujenzi wa barabara hizo unavyounganisha nchi za EAC na kuchochea biashara, mwingiliano wa watu ili kuimarisha mtangamano.

 

Wajumbe wa kamati hiyo ambao pia walitembelea Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Namanga, walisikiliza mada kutoka kwa Mkurugenzi wa Miundombinuya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eliabi Chodota.

 

Mada hiyo pamoja na mambo mengine ilieleza miradi mingine inayotekelezwa kwa uratibu wa EAC katika sekta za usafiri wa anga, reli, majini; hali ya hewa na nishati katika nchi wanachama.

 

&&&&&&&&&&&&&&&

 

 

Viongozi Afrika wajadili kukabili mabadiliko tabianchi

Na Mwandishi Wetu

 

 

WAZIRI wa Nishati, January Makamba amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa viongozi wa dunia unaojadili programu ya Afrika kukabili mabadiliko ya tabianchi.

 

Mkutano huo unaofanyika Rotterdam, Uholanzi, unalenga kushawishi washirika wa maendeleo, taasisi za kifedha na sekta binafsi na marafiki wa Afrika kuchangia fedha kwenye Programu hiyo ya Afrika ambayo inahitaji Dola za Marekani bilioni 25 ifikapo 2025.

 

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imechangia Dola za Marekani bilioni 12.5. Mkutano huo unafanyika kama sehemu ya maandalizi Mkutano wa 27 Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu Sharm El Sheik, Misri.

 

January amekutana na viongozi wa dunia, wakuu wa taasisi na mashirika kujadili fursa zikiwamo namna bora ya Tanzania kunufaika na mpango huo utakaoharakisha mipango ya nchi katika kukabili majanga yakiwamo Covid-19, ukame, njaa, ajira kwa vijana na mafuriko.

 

Mkutano huo uliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Macky Sally na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (GCA), Ban Ki-Moon.

 

Septemba 2, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alisema Tanzania ipo tayari kushiriki katika jitihada za kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.

 

Balozi Mulamula alitoa kauli hiyo Dar es Salaam wakati wa kufunga Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ulioandaliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Uingereza na kushirikisha nchi 20.

 

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&

 

 

Watu wawili wauawa kambini TFS

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

 

WATU wawili wamekufa na wengine sita wamejeruhiwa baada ya watu wanaoaminika ni wafugaji kuvamia kambi ya Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwenye Kijiji cha Mvinza Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Filemon Makungu alisema mjini Kigoma jana kuwa uvamizi huo ulifanyika kwenye kambi hiyo iliyopo kwenye Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini mwishoni mwa wiki iliyopita.

 

Kamanda Makungu aliwataja waliokufa kuwa ni mkazi wa Kijiji Mvinza aliyejulikana kwa jina moja la Salvatory ambaye alikuwa kibarua kwenye shamba hilo la miti la TFS ambaye alichomwa na vitu vyenye ncha kali.

 

Aidha, alisema juzi polisi wakiwa kwenye ukaguzi wa eneo hilo kuangalia athari ya tukio hilo, maiti ya mtu mwingine ilipatikana, Thomas Alfred aliyekuwa akifanya kazi za vibarua kwenye kambi hiyo ya TFS. Mwili wake ukiwa na majeraha makubwa shingoni.

 

Aliwataja waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni Dora Nicolaus na David Lazaro ambao ni watumishi wa Suma JKT wakiwa kwenye kazi ya ulinzi ya kambi hiyo, Amon Moshi mtunza bustani, Ndayishimiye Haruna mkulima wa bustani na Elcado Enos pia mkulima.

 

Mbali ya mauaji na watu hao kujeruhiwa, pia vitu mbalimbali vimeteketezwa kwa moto likiwamo trekta mali ya TFS, nyumba moja ya tofali za kuchoma iliyoezekwa na bati ikitumika kama ofisi, pikipiki sita za watuhumiwa waliokamatwa kwa kuingia kwenye hifadhi ya msitu kinyume cha sheria, gunia 20 za maharage, gunia 70 za mahindi, gunia 30 muhogo na gunia 20 za mtama.

 

“Taarifa za awali zinaonesha kuwa siku za karibuni kuna ng’ombe ambao idadi bado haijajulikana ya wafugaji jamii ya Wasukuma walikamatwa na kuchukuliwa na maafisa wa TFS kwa tuhuma za ng’ombe hao kuingizwa kwenye hifadhi ya msitu kwa ajili ya malisho.

 

“Hivyo vurugu hizo zimekuja kama nia ya watu hao kulipiza kisasi kwa mifugo yao kukamatwa na ndiyo maafa hayo yametokea,” alisema Kamanda Makungu.

 

Watu watatu wanaoaminika ni sehemu ya wafugaji hao, wamekamatwa na wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo na uchunguzi unaendelea.

 

****************tamati****************

1 comments

Comments are closed.