Waliokufa ajalini Tanga wafika 20

IDADI ya watu waliokufa katika ajali iliyotokea wilayani Korogwe mkoani Tanga imeongezeka kutoka 17 hadi 20.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba alisema hayo jana wakati wa ibada ya kuaga miili ya watu 16 katika hospitali ya Magunga wilayani Korogwe.

Mgumba aliwaeleza waombolezaji kuwa majeruhi waliopoteza maisha usiku wa kuamkia leo walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam na Hospitali ya mkoa wa Tanga ya Bombo.

Waliokufa kwenye ajali hiyo ni Doris Mrema, Tony Mrema, Atanas Mrema, Augustino Mrema, Eveline Mrema, Kennedy Mrema, Godwin Mrema, Zawadi Mrema, Elizabeth Mrema, Julieth Mrema , Cosmas Mrema na Rajab Mrema.

Marehemu wengine ni Rozina Lames, Festo Ndunguru na Yussuf Saimon, Eluminata Silayo na Festo Mwambungu.

“Jana (juzi) tulisafirisha majeruhi wawili akiwemo mtoto mmoja kwenda Muhimbili kwa àjili ya matibabu zaidi lakini nasikitika kusema kuwa tumepata taarifa kuwa amefariki na wengine wawili waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya Bombo nao wamepoteza maisha”alisema.

Aidha Mgumba alitoa ufafanuzi kuhusu agizo la kuwasimamisha kazi watumishi wawili wa idara ya afya ili kupisha uchunguzi wilayani humo kwa kuwa walichelewa kwa saa nne kufika hospitali ya Magunga kuhudumia majeruhi.

Aliwataja waliosimamishwa kuwa ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Salma Swedi na Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Magunga, Dk Heri Kiwale.

“Ajali imetokea saa nne na nusu mpaka saa tano na robo majeruhi walikuwa wameshafika Magunga lakini watumishi hao walifika kuanzia saa 10.45 alfajiri wakati wanaishi jirani na hospitali, hili lazima wasimame kwanza ili kupisha uchunguzi”alisema Mgumba.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kalist Lazaro alisema baada ya ibada ya mazishi jana miili ingesafirishwa kupelekwa wilayani Rombo kwa ajili ya mazishi na maziko.

Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Dk Abubakar Zubeir amewataka Watanzania wawe wavumilivu na wamtangulize Mungu kwa kila jambo likiwamo la huzuni kama hilo.

Mufti alisema msiba huo ni mkubwa na umegusa mioyo ya Watanzania hivyo ni wakati wa moyo ya uvumilivu na ustahamilivu na kumtegemea Mungu.

Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maaskofu na mashehe ya maadili, amani na haki za binadamu kwa jamii za madhehebu ya dini nchini, Askofu William Mwamalanga amehimiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wahakikishe barabara zina alama za barabarani.

Ndugu wa marehemu waliishukuru serikali kwa namna ya walivyosaidia tangu ilipotokea ajali juzi Februari 6 saa 4.30 usiku katika eneo la Magila Gereza wilayani Korogwe katika barabara kuu ya Barabara Kuu ya Segera – Bwiko.

“Tunaishukuru sana serikali kwa namna walivyoweza kutusaidia katika kipindi hiki kigumu, huu ni msiba ni mkubwa sana kwetu”alisema Gines Mrema.

Ndugu mwingine wa marehemu, Athanas Mrema alisema tukio hilo la vifo vya watu 13 ni pigo kubwa kwa familia yao.

Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 673 CUC lilipogongana uso kwa uso na Toyota Coaster lenye namba za usajili T 863 DXN ikiwa imebeba mwili wa marehemu na waombolezaji wakienda kuzika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Habari Zifananazo

Back to top button