Waliomaliza kidato cha sita 2024 waitwa JKT

DODOMA: JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limewaita vijana waliohitimu kidato cha sita mwaka 2024 kutoka shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya JKT Chamwino mkoani Dodoma, Brigedia Jenerali Hassan Mabena alisema tayari jeshi hilo limewapangia makambi vijana wa kundi la lazima watapatiwa mafunzo.

Alisema vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia Juni Mosi hadi Juni 7, mwaka huu.

Brigedia Jenerali Mabena alisema vijana hao wamepangwa katika Kambi za JKT Rwamkoma -Mara, JKT Msange – Tabora, JKT Ruvu – Pwani, JKT Mpwapwa, Makutupora JKT- Dodoma na JKT Mafinga – Iringa.

Makambi mengine waliyopangiwa ni JKT Mlale – Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba – Tanga, JKT Makuyuni – Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila – Kigoma, JKT Itaka- Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa – Rukwa, JKT Nachingwea – Lindi, JKT Kibiti – Pwani na Oljoro JKTArusha.

Aidha, aliwataka vijana wa kundi la lazima watakaohudhuria mafunzo hayo kuripoti wakiwa na vifaa mbalimbali vikiwemo bukta ya rangi ya buluu iliyokoa yenye mpira kiunoni, mfuko mmoja nyuma na urefu unaoishia magotini na isiyo na zipu.

Pia, aliwataka wafike na fulana ya rangi ya kijani, raba za michezo rangi ya kijani au buluu, shuka mbili za kulalia zenye rangi ya buluu bahari, soksi ndefu za rangi nyeusi na suti za michezo (tracksuit) ya rangi ya kijani au buluu.

Alisema vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini wakiwa na nakala za nyaraka zote zinazohitajika katika udahili wa kujiunga na elimu ya juu, zikiwemo cheti cha kuzaliwa, vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na nauli ya kwenda makambini na kurudi nyumbani.

“Orodha kamili ya majina ya vijana hao, makambi ya JKT waliyopangiwa na maeneo makambi hayo yalipo na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo, inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz,”

Habari Zifananazo

Back to top button