Waliorasimisha ardhi wakopeshwa bil 42/- 

ZAIDI ya Sh bilioni 42.02 zimekopwa kutoka taasisi mbalimbali za fedha na wamiliki wa ardhi iliyorasimishwa kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA).

Akizungumza jijini hapa, Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge, Dk Seraphia Mgembe alisema waliokopeshwa kiasi hicho cha fedha ni wamiliki wa ardhi iliyorasimishwa wapatao 2,690.

Alisema kwa upande wa urasimishaji ardhi vijijini, mashamba 187,887 yamepimwa ambapo hati miliki 101,103 zimetolewa.

Dk Mgembe alisema mpango huo pia umewezesha ujenzi wa masjala za ardhi vijijiji 42 ambazo kwa sasa zimekamilika huku masjala sita zikiwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji na kwamba masjala za ardhi za wilaya mbili zimekarabatiwa.

Alisema kupitia mpango huo katika suala la kuwajengea uwezo wameweza kuzifikia halmashauri 63, kata 370 na vijiji 534 ambapo viongozi wa halmashauri waliojengewa uwezo ni 630, viongozi wa kata 370 na viongozi wa vijiji ni 675.

Alisema pia Mkurabita imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa matumizi ya kiuchumi ya hati miliki za kimila kwa wananchi ambao ardhi yao imerasimishwa na kuwaunganisha na fursa za mitaji ambapo halmashauri 25 zimefikiwa na wakulima na viongozi 9,400 wamepata mafunzo hayo.

Dk Mgembe alisema kwa upande wa urasimishaji ardhi mijini, mpango huo umefikia kwenye halmashauri 11 za Tanzania Bara ambapo viwanja vilivyopimwa ni 30,569 na hati miliki 5,496 zilizotolewa.

Alisema kwa upande wa Zanzibar, mpango huo umefikia wilaya tano za Unguja na Pemba ambapo viwanja vilivyopimwa ni 24,320 na hati miliki 8,589 za matumizi ya ardhi zilizotolewa.

Akizungumzia matokeo ya mpango huo baada ya kufanya tathmini ya ndani, Dk Mgembe alisema mpango huo umesaidia kuongeza thamani ya ardhi na kuongeza tija katika uzalishaji pamoja na kuongezeka kwa wakopaji katika taasisi za fedha.

Pia alisema kumekuwapo na kupungua kwa migogoro ya ardhi na kwamba wananchi waliorasimisha ardhi yao wameongeza usalama wa milki.

Habari Zifananazo

Back to top button