Waliosimamishwa kazi na Waziri Mkuu wafikishwa mahakamani

Watumishi wawili akiwemo Mkurugenzi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mpanda (MUWASA) Hussein Nyemba na Kaimu Afisa Utumishi wa (MUWASA) Justine Wambali wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka mawili ikiwemo kutumia vibaya madaraka na kuisababishia mamlaka hasara.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imeanza kusikilizwa leo disemba 29,2022 katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda ikiwa ni siku 17 toka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuiagiza TAKUKURU kumfanyia uchunguzi Mkurugenzi wa Maji safi na usafi wa mazingira Mpanda (MUWASA) Hussein Nyemba wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Mkoa wa Katavi katika ukumbi wa mikutano wa Mpanda Manicipal Social Hall mnamo Disemba 12,2022.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Stuart Kiondo amesema watuhumiwa wote wanashitakiwa kwa kutumia vibaya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU CAP. 329 marejeo ya 2022.
“Justine Wambali yeye ameingia kwa sababu ni afisa utumishi na anawajibika tangu mwaka 2016 yeye alikuwa ni kaimu afisa utumishi wa MUWASA na anapaswa kuwajibika kutokana na shauri ambalo tumelipeleka mahakamani kuhusiana na ajira ya watumishi 37 bila kufuata utaratibu”
Aidha, Kiondo amesema mashitaka mengine wanayokabiliwa nayo ni kuisababishia mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Mpanda (MUWASA) hasara ya kiasi cha Tsh. 17,817,000/- kinyume na kifungu cha 284A (1) kanuni ya adhabu sheria No. 16.
Hata hivyo, Hussein Nyemba amefanikiwa kupata dhamana baada ya kukidhi vigezo ambapo masharti ya mdhamana kwenye kesi hiyo ilikuwa kila mmoja awe na mdhamini mwenye mali isiyo hamishika yenye thamani ya shilingi milioni tano na barua kutoka kwenye mamlaka zinazotambulika na Serikali.