Waliotelekeza vibanda vyao SIMU 2000 warejea

DSM: WAFANYABIASHARA waliotelekeza vibanda vyao katika Soko la Simu 2000 mkoani Dar es Salaam, wameanza kurudi kutokana na maboresho yaliyofanyika.

Mfanyabiashara katika soko hilo, Charles Goodluck amesema hayo alipozungumza na HabariLeo ili kupata maoni yake kutokana na maboresho yanayoendelea sokoni hapo.

Amesema wafanyabiashara wameanza kurejea kwa kuwa waliondoka kwa kuwa soko hilo halikuwa na mazingira rafiki hususan katika kipindi cha mvua.

Katika hilo, ameipongeza Manispaa ya Ubungo kwa Ushirikishwaji wa wafanyabiashara juu ya namna bora ya kuboresha soko hilo kwa kuzingatia mahitaji yao ambapo vibanda vilivyojengwa vinamuwezesha mteja kufika kwenye kila kibanda kutokana na jinsi vilivyojengwa.

Kwa upande wake mfanyabiashara Zainab Hassan amesema uboreshaji wa soko hilo pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara utaiwezesha Manispaa kuongeza mapato yake.

“Sisi kama wafanyabiashara kwa maboresho haya tupo radhi tena kwa hiari kulipa ushuru na kodi mbalimbali za Manispaa kwani tunaona matunda yake” amesema.

Naye Ofisa Mfawidhi kutoka Manispaa ya Ubungo, sehemu ya biashara na masoko, Geofrey Mbwama amesema hatua hiyo ni katika kutekeleza sera na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha masoko yanaboreshwa.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Manispaa ya Ubungo imeweza kutenga zaidi ya Sh bilioni mbili ambazo ni za mapato yake ya ndani kwa ajili ya uboreshaji wa masoko ikiwemo soko la Mabibo, soko la SIMU 2000, soko la Manzese na soko la Mbezi Shule ili kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.

Kuhusu ujenzi wa vibanda amesema kwa mara ya kwanza manispaa hiyo imetenga
Sh milioni 100 kwa ajili ya uboreshaji wa vibanda vya soko hilo.

Jumla ya vibanda 170 vimejengwa na kwa awamu ya pili kiasi cha Sh milioni 39 kwa ajili ya ujenzi wa vibanda 80 vya wafanyabiashara.

Soko la SIMU – 2000 ni miongoni mwa masoko 13 yanayomilikiwa na Manispaa ya Ubungo ambalo lilianzishwa mwaka 2014 likiwa limejengwa vibanda 312 na baadae wafanyabiashara walihamishwa kutoka kwenye maeneo mbalimbali waliyokuwa wakifanyia biashara ambayo hayakuwa rasmi na kuhamishiwa sokoni hapo lakini walitelekeza vibanda vyao kutokana na hali iliyokuwa hapo awali.

Habari Zifananazo

Back to top button