MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema ifikapo Novemba Mosi mwaka huu serikali itajitoa kuwadhamini wananchi 3,881 ambao walivamia eneo la Kiwanda cha Wazo endapo hawatalipa kama walivyoelekezwa.
Makalla alisema hayo alipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kupata taarifa ya wananchi waliolipa toka walipoagizwa kufanya hivyo miezi sita iliyopita.
Alisema kati ya wananchi 4,070 waliovamia eneo hilo waliolipa fidia ni 39, sawa na asilimia tisa idadi ambayo ni ndogo na kwamba watu 150 wamelipa kiwango cha kupata hati na sio fidia na waliobakia 3,881 hawataki kulipa.
“Serikali ilishawishi Wazo irasimishe eneo hilo ili watu wasiondolewe bali walipe fidia ambapo kwa sq meta moja Sh 6,419,” alisema Makalla.
Alisema baada ya watu hao kukaidi wametoa nafasi nyingine kwao waweze kupokea ankara ili waweze kulipa.
Makalla alisema baada ya hapo watawakabidhi watu hao kwa kiwanda cha Wazo ili kiendelee na hatua nyingine.
Mkazi wa Wazo Chatembo, Fatma Salehe alisema serikali ikisema hawawezi kapinga, hivyo watajitahidi kulipa japo hali ni ngumu.