Waliowekewa magoti, nyonga bandia waruhusiwa Mloganzila

BAADHI ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kuweka magoti na nyonga bandia katika kambi maalumu inayoendelea Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila wameanza kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya afya zao kuimarika.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo leo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila Dk Godlove Mfuko ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji amesema kuruhusiwa kwa wagonjwa hao kunadhihirisha namna Mloganzila ilivyokidhi viwango vya kimataifa vya kufanya aina hiyo ya upasuaji.

“Kwa viwango vya kimataifa mtu aliyefanyiwa aina hii ya upasuaji kama hakuna dharura yoyote huwa ni siku tatu hadi tano, kwa hiyo na sisi tunakwenda na viwango hivyo ambapo wagonjwa walifanyiwa Jumatatu leo wanaruhusiwa,” amesema.

Dk Mfuko amebainisha kuwa mbali na kupata wagonjwa kutoka karibia mikoa yote ya Tanzania, pia alipatikana mgonjwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), jambo ambalo linaonesha kuwa kambi siyo tu imenufaisha Watanzania bali hata raia kutoka nchi ya kigeni.

Kwa upande wake kiongozi wa kambi hiyo Prof. Mamoun Gadir kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth nchini Uingereza amesema kuwa mpangilio na muundo wa hospitali ya Mloganzila hauna tofauti za hospitali za nchi zilizoendelea na kwamba wataalamu wanayo maarifa ya msingi hivyo wakiongezewa maarifa za ziada kidogo tu wanaweza kuwa wabobezi.

Aidha ameshauri Hospitali ya Mloganzila kuwa kituo maalumu cha kutoa matibabu ya nyonga na magoti.

Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa nyonga na magoti MNH-Mloganzila Dk Shilekilwa Makira amebainisha sababu mbalimbali zinazofanya maradhi ya nyonga na magoti kuwa ni pamoja na umri mkubwa, maradhi ya selimundu, pumu ya mifupa na ajali.

Amesema kuwa kambi hiyo mbali na kutoa huduma pia imetoa fursa kwa wataalamu kutoka hospitali za Temeke RRH, CCBRT na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH) kujifunza, pia ametoa shukrani kwa wataalamu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushiriki kuwajengea uwezo.

“Baada ya kambi kuisha utaratibu wa matibabu kwa watu wenye changamoto za nyonga na magoti utaendelea kama kawaida ambapo tutawaona katika kliniki zetu na kama wataonyesha wanahitaji upasuaji tutawafanyia” amesema Dk Makira.

Kambi hiyo maalumu ilianza Novemba 27 mwaka huu imeratibiwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Global Medicare, ambapo hadi leo watu 14 wamenufaika na upasuaji huo ambapo hadi kufikia Disemba Mosi mwaka huu watu 35 wanategemewa kufanyiwa.

Habari Zifananazo

Back to top button