Walipwa fidia Mtwara baada ya miaka 22

BAADA ya vilio, malalamiko na madai ya wananchi wa Mangamba Juu, Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara kwa serikali wakidai fidia ya maeneo yao kwa takribani miaka 22, hatimaye wametabasamu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa kutoa Sh 816,786,000, kuwalipa fidia.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Danstan Kyobya, alitoa taarifa hiyo jana kwa wananchi hao na kueleza kuwa wananchi wa Mangamba Juu walitoa eneo lao miaka 22 iliyopita  kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA), kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji.

“Mheshimiwa Raisi ameleta shilingi milioni mia nane, kumi na sita, laki Saba na themanini na sita elfu, ambazo zitalipwa kama fidia kwa eneo la wananchi lililochukuliwa kwa ujenzi wa miundombinu ya maji ya MTUWASA hapa Mtwara,” amesema.

Kyobya ameshukuru Rais Samia na Waziri wa Maji Jumaa Aweso, pamoja na mamlaka ya maji kwa kutoa fidia hiyo, ambayo wananchi walidai kwa takribani miaka 22.

“Nikupongeze Mkurungenzi wa MTUWASA pamoja na watendaji wote kwa kuwa najua ndani ya miaka hii 22, cha moto mmekiona, malalamiko ya wananchi, maombi vilio,” amesema na kuwapongeza wananchi hao kwa kuwa wavumilivu.

Kyobya amewataka MTUWASA waanze jana Jumamosi kulipa fidia hiyo kwa wananchi, huku akiwataka wananchi wanaostahili kulipwa kuhakikiwa upya kabla ya malipo.

“Kila mwananchi ambaye yupo kwenye orodha ya kulipwa fidia ahakikiwe kabla ya malipo kujua kama ni yeye au siyo yeye,” amesema na kuwataka wananchi wanaostahili malipo hayo kuwa na akaunti benki, ili fedha ya fidia yao ipelekwe benki.

Habari Zifananazo

Back to top button