KUANZIA leo wamachinga katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wanaanza kuhamia kwenye soko jipya la kisasa ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, amesema wafanyabiashara hao wameanza kuhamia katika soko jipya kuanzia jana na mpaka Septemba 23 mwaka huu, wote watakuwa wamehamia kwenye soko hilo.
“ Kuanzia leo wafanyabaishara wataanza kuhamia na hadi kufika Septemba 23 mwaka huu wote watakuwa wamehamia kwenye soko na Septemba 24 tutafanya usafi mkubwa, ambao utaliacha Jiji la Dodoma likiwa katika hali ya usafi.
“ Katika utaratibu huu wa kuwahamisha wafanyabiashara hao, hakuna mmachinga ambaye atapigwa virungu au kusukumwa, tunataraja baada ya muda huo kufika hakuna biashara ya wafanya biashara wadogo itafanyika nje ya soko na hakuna biashara itakayofanyika mbele ya duka,” amesema.

Amesema kujengwa kwa soko hilo kutawaongezea usalama wateja na watoa huduma, ambao wanafanya biashara hizo na kuwapa maeneo salama ya kufanyika biashara zao.
“ Wamachinga wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali, jua lao, mvua yao na hata usalama wa bidhaa zao ulikuwa mdogo, lakini kwa miundombinu hii tunakwenda kuongeza usalama wa wamachanga na wateja wao.
“ Kwa sasa kama mteja amenunua sweta kwenye kibanda D2, na kufika nyumbani akakuta limechanika, ataweza kulirejesha kwa sababu aliponunua panajulikana na aliyeuza tumemsajili na taarifa zake ziko ofisini, ” amesema.