Wamiminika Mloganzila kuweka puto
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila jijini Dar es Salaam inatarajia kutoa huduma ya kupunguza uzito kwa watu zaidi ya 10 katika kambi ya siku nne ambayo imeanza leo na kuhitimishwa January 23,2023.
Tangu kuanza kwa huduma hiyo Novemba mwaka jana, jumla ya watu 26 wamepunguzwa uzito mkubwa/uliokithiri.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Januari 20,2022 Naibu Mkurugenzi wa Mloganzila Dk Julieth Magandi alisema wamejipanga kikamilifu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa wakati.
“Huduma hii inahusika na kuweka puto tumboni bila upasuji kwa wagonjwa ambao wanauzito uliopitiliza kiwango kinachotakiwa na tumejipanga kuanzisha huduma hii katika mifumo miwili wa kwanza tumeanzisha kliniki maalum ya wagonjwa wote lazima wapime kiwango cha mafuta katika damu na kwa wale ambao wanataka kupunguza uzito wataonana na timu ya wataalam kuhudumiwa,”amesema
Dk Magandi amesema huduma hiyo ndani ya nchi inagharimu kiasi cha Sh milioni 4 hadi 4.2.
Amesema mgonjwa anapofika moja kwa moja anapelekwa chumba maalum na wataalamu wote wanaotakiwa watamuona na huduma atapewa akiwa sehemu moja.
Aidha, amebainisha kuwa tangu wameanza mwitikio umekuwa mkubwa sana na kusababisha kuanzisha kambi maalum ambapo kwa siku ya jana wagonjwa sita walipata huduma.
Pia ametoa wito kwa mwenye uhitaji wa huduma afike Mloganzila atapata huduma nzuri.
” Tukumbuke watu walikuwa wanasafiri kwenda nje lakini sasa huduma ipo ndani,
wataalmu wapo wakutosha na vifaa vipo mgonjwa akija asubuhi jioni anatoka.
Amesema lengo la huduma hiyo ni kuunga mkono serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.