WAFUGAJI wanaoishi kijiji cha Oltepesi wilayani Longido wamemshukuru Rais Samia Hassan Suluhu kwa ujenzi wa shule ya sekondari ya Wasichana ya Orbomba yenye thamani ya Sh bilioni 3 kupitia mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari Nchini (SEQUIP).
Shukrani hizo zimetolewa na Lens’unini Marle mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,John Mongella kutembelea eneo hilo kwaajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo ya kisasa ya sayansi itakayowezesha kuibua vipaji vya watoto wakike na kuzalisha wataalam katika sekta mbalimbali nchini.
Marle amesema shule hiyo itakuwa chachu kwa jamii ya wafugaji mara itakapokamilika kwani itaondoa dhana ya kudharau watoto wakike ambao awali jamii za wafugaji zilikuwa haziwapi msukumo katika elimu na badala yake wazazi au walezi kukimbilia kuwaozesha.
“Shule hii itakapokamilika Disemba mwaka huu ,itafungua dunia na kuonyesha watanzania na jamii ya wafugaji kuwa elimu ndio msingi kwa mtoto wa kike na sasa hivi tunaona wanawake wanafanya vema katika nafasi mbalimbali wanazopewa na tunaamini hata hapa shule ikikamilika wanafunzi wa kike wataonyesha uwezo wao mkubwa katika masomo”
RC Mongella amepongeza kasi kubwa ya ujenzi wa shule hiyo inayosimamiwa na kamati ya ujenzi inayojumuisha vyumba 12 vya madarasa, mabweni 8,maabara 2 za masomo ya sayansi, jengo la utawala, nyumba mbili za walimu, maktaba, chumba cha TEHAMA, chumba cha wagonjwa pamoja na matundu 12 ya vyoo.