Wamuenzi Nyerere kwa usafi Zahanati Sombetini

TAASISI ya Bethany International Services, imemuenzi hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa kufanya usafi Zahanati ya Sombetini jijini Arusha na kutoa msaada wa vifaa tiba.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Jimmy Pamba amesema wameamua kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo zaidi, ikiwemo kutoa misaada kwa jamii, ili kusaidia huduma za afya katika kituo hicho.

“Lazima vijana tuamke kusaidia jamii kadri tunavyoguswa, kwani jamii ina mahitaji mengi na ni vema kuwasaidia,”amesema na kutaja vifaa tiba walivyosaidia kuwa ni vifaa vya kupimia mapigo ya moyo pamoja na mashine ya kupima misuli na hewa.

Kwa upande wake Katibu wa taasisi hiyo, Abdillah Lugome, alisema wametumia siku hiyo kwa ajili ya kufanya usafi vyooni, upandaji wa miti aina ya chaya, ili kusaidia wananchi wenye uhitaji na kutoa vifaa tiba.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, muuguzi wa hospitali hiyo, Sarfonia Mlay alishukuru kwa msaada huo na kutoa rai kwa jamii kuendelea kushirikiana nao kwa misaada mbalimbali, ili kuboresha huduma za afya.

Habari Zifananazo

Back to top button