Wamuomba Rais Samia kulipwa fidia zao

WAKULIMA na wafugaji zaidi ya 120 kutoka kijiji cha Lolkisale Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha wamemuomba Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani kuwasaidia kulipwa fidia ya mashamba yao ekari 47,000 kubadilisha matumizi ya kilimo na ufugaji kwenda jeshini.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Arusha ,katibu wa wakulima hao, Joseph Ngaluko alisema wana hati ya ardhi ya umiliki wa mashamba hayo iliyotolewa mwaka 1990 na Halmashauri ya Wilaya ya Monduli na wana nyaraka za nakala za barua zinazoonyesha wanapaswa kulipwa fidia baada ya serikali kubadilisha matumizi ya ardhi hiyo mwaka 2003.

Ngaluko alisema wanaamini Rais ana hofu ya Mungu na mpenda haki na kamwe hapendi serikali yake kudhurumu wananchi wake kwani hadi sasa ni zaidi ya miaka 20 wakulima hao wanaisaka fidia serikalini na kibaya zaidi na cha kusikitisha wakulima zaidi ya 20 wamefariki huku wakihangaika kusaka fidia hiyo.

Alisema kwa muda wote waliokuwa wakihangaika kusaka haki yao hawajawahi kukosa kuingia katika ofisi zote za serikali kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na Wizarani na ofisi zote wamekiri wanastahili kulipwa fidia kwa kuwa serikali ndio ilitwaa ardhi yao na kubadilisha matumizi lakini utekelezaji wa fidia hiyo ndio umekuwa danadana hadi sasa.

‘’Tunakuomba Rais usikilize kilio chetu cha fidia ya mashamba yetu yaliyopo Loksale Wilayani Monduli kwani wanastahili kulipwa kwa kuwa ni haki yao na serikali ilitwaa mashamba hayo mwaka 2003 na kukiri kulipa lakini hadi sasa hatujalipwa ‘’

‘’Hakuna ofisi ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi{CCM} isiyokuwa na taarifa juu la malalamiko yao fidia lakini utekelezaji ndio changamaoto hivyo wewe kama Rais wetu tunaomba msaada wako juu ya hili’’alisema Ngaluko

Naye mhanga mwingine wa mashamba hayo aliyejitambulisha kama mjumbe wa kamati, Donald Mmari yeye alisema kuwa wakulima wote wanahati miliki za mashamba hayo na hati zao hazijawahi kufutwa na serikali hadi sasa kubadilisha matumizi ya ardhi ya mashamba hayo kutoka kilimo na ufugaji kwenda JWTZ.

Mmari alisema mwaka 1988 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ilitoa tangazo la kugawa ardhi eneo la Lolkisale kwa watu wa ndani ya wilaya hiyo na nje na wananchi waliomba kwa barua na wakati huo Mwenyekiti wa ugawaji ardhi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri,Methew Gard.

Alisema mwaka 1990 Kamati ya ugawaji ardhi ilikuwa chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Monduli kipindi hicho,Elly Nyagawa na mwaka 1991 Kamati ya ugawaji ardhi ilikuwa chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Monduli kipindi hicho Kanali Enos Mfuru.

Mmari alisema kuwa kila aliyefanikiwa kupewa ardhi katika eneo la Lolkisale alipewa nakala ya barua na kuonyeshwa eneo lake na pia alipaswa kumgharamia mpimaji kwa ajili ya kupimiwa eneo hilo lakini ghafla mwaka 2003 wakiwa na nyaraka zote za umilikiwa wa mashamba hayo walikuta tangazo likisema ‘’Hatari Usiingie Eneo la Mafunzo ya JWTZ’’

Alisema kuwa walikuwa wakilima na kufuga kwa zaidi ya miaka 13 katika mashamba hayo eneo la Lolkisale na hawana shida na serikali kuamua kubadilisha matumizi ila wanashida na kutaka fidia ya mashamba hao na sio vinginevyo.

Mjumbe huyo alisema ziliundwa kamati zaidi ya nne mbili za wilaya na mkoa na mbili za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa lakini kamati zote hizo hazijawahi kuweka wazi uchunguzi wao mbali ya kuja eneo na kuhoji wakulima na watendaji wa Halmashauri ya Monduli.

Habari Zifananazo

Back to top button