Wanafunzi 12,000 kujengewa uwezo kazi za ujuzi

KIGOMA: Zaidi ya Sh bilioni 67 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuwezesha wasichana wadogo na walemavu  kupata elimu na ujuzi  vitakayowezesha wasichana na wenye changamoto mbalimbali kupata kazi za staha na zenye ujuzi baada ya masomo yao.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Serikali ya Ubelgiji nchini Tanzania (ENABEL), Koenraad Goekint wakati wa uzinduzi wa mradi wa miaka mitano unaojulikana kwa jina la WEZESHA BINTI ambao utatumika kuinua uwezo wa wasichana na wenye changamoto kielimu.

Koenraad alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo jumla ya shule za sekondari 25 katika Mkoa wa Kigoma zitafikiwa ambapo wanafunzi wasichana na wanafunzi wavulana wenye changamoto 12,750 watafikiwa.

Advertisement

Amesema kuwa katika shule hizo 25 shule nane zitajengewa mabweni yatakayokuwa na kila kitu kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi hao ikiwemo mfumo wa teknolojia ya kompyuta,shule kuwekewa  mfumo wa vyoo vya kisasa vyenye mfumo wa maji safi na maji taka huku walimu 500 wa sekondari wakipatiwa mafunzo kwa ajili ya kuwezesha kufundisha masomo ya hisabati na sayansi.

Akizungumza wakati akizindua mradi huo Mkuu wa Mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema mradi huo ni muhimu kwa Mkoa wa Kigoma katika kuinua hali za wasichana kielimu lakini kuwasaidia kuingia kwenye soko la ajira wakiwa na ujuzi ambao hautawafanya kuwa watu wa kuomba kusaidiwa.