14,766 wapatiwa mafunzo ugunduzi teknolojia

DAR ES SALAAM; JUMLA ya wanafunzi 14,766, wamepatiwa mafunzo ya ugunduzi wa teknolojia kupitia mpango wa mafunzo ya utafiti wa kisayansi shuleni kuanzia mwaka 2012.

Kwa upande wa walimu waliopatiwa mafunzo chini ya mpango huo ni 2395 katika shule mbalimbali za sekondari nchini, jambo linaloongeza mwamko wa wanafunzi kupenda masomo hayo.

Mwanzilishi Mwenza wa Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi (YST), Dk Gozibert Kamugisha amesema hayo leo Dar es Salaam na kuongeza kuwa mwaka 2024 jumla ya maombi 1,042 ya kazi za kisayansi yamewasilishwa ili kushindanishwa na wanafunzi watakaoshinda kupata udhamini wa masomo vyuo vya elimu ya juu.

Advertisement

Amesema kazi za kisayansi na teknolojia zitakazooneshwa mwaka huu ni za aina mbalimbali, zikiwemo zilizojikita kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi, nishati, uzalishaji na utunzaji usalama wa chakula.

Amesema zipo kazi za teknolojia za kubadili tabia za madereva, ili kupunguza ajali za barabarani, teknolojia za kukabiliana na upotoshaji wa habari, kiwango cha usalama wa chakula kinachotumiwa na wanafunzi shuleni.

Amesema shule zenye klabu za sayansi zimeonesha kushiriki vyema katika mafunzo ya ugunduzi wa teknolojia na kutoa wito kwa shule nyingine kuifikia fursa hiyo kwa maendeleo ya sayansi nchini.

Amesema kwa miaka 13 iliyopita wanafunzi 45 wamepewa ufadhili wa masomo ya chuo kikuu kusoma masomo ya sayansi na teknolojia, mbali na kuendelea na masomo yao ya vyuo baadhi yao wameendeleza ugunduzi wao na kuzifanya bidhaa za kuuzwa kwenye soko.

“Mfano wa gunduzi zilizoendelezwa ni pamoja na ile ya kubaini na kutoa taarifa za majanga ya moto majumbani kwa kutumia simu ya mkononi, matumizi ya virutubisho vya mmea wa mbigiri katika ufugaji wa wanyama, matumizi ya mmea wa kivumbasi katika ufugaji wa nyuki,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya Karimjee Foundation, Caren Rowland amesema wamekuwa wakishirikiana na YST kuchochea ukuaji wa sayansi na teknolojia katika jamii.