WANAFUNZI 48,621 kutoka shule 68 wamenufaika na mpango wa unywaji maziwa shuleni ambayo yamekuwa yakitolewa kwa ushirikiano na serikali, wazazi, wafadhili mbalimbali na wasindikaji wa maziwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alitaja idadi hiyo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya unywaji maziwa shuleni iliyofanyika Nyerere Square jijini hapa.
Alisema hadi kufikia jana ni shule 68 zenye idadi ya wanafunzi 48,621 zilizonufaika katika mpango wa unywaji maziwa shuleni.
“Ongezeni juhudi zaidi ili wanafunzi wote wafaidike na mpango huu hapa nchini. Juhudi hizi ziende sanjari na kuongeza uzalishaji wa maziwa ambao kwa sasa umefika lita bilioni 3.4 (kwa mwaka),” alisema.
“Tunahitaji kujenga utamaduni wa kunywa maziwa na mazao yake kama vile mtindi, siagi na jibini kwa ajili ya kuboresha afya zetu. Nitoe rai kwa Watanzania wa rika zote kunywa maziwa ya kutosha kwa ajili ya afya zetu,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema umuhimu wa maziwa hauishii tu kwenye afya bali ni tasnia muhimu katika kujenga uchumi wa viwanda na hivyo kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla.
Alifafanua kwamba maziwa ni zao la kwanza katika mazao ya kilimo lenye mzunguko mkubwa kibiashara na kwamba mfugaji anayejihusisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kila siku ana uhakika wa kupata kipato.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha kuwa kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa na wenye tija kwa wananchi ili kutoa mchango unaostahili katika kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
Alitoa rai kwa wafugaji nchini kuunda ushirika imara utakaowawezesha kupata huduma mbalimbali za mifugo na ushirika huo ulenge katika kuboresha uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa, upatikanaji wa masoko pamoja na kuongeza kiasi cha usindikaji viwandani.
“Nitoe wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinawezesha na zinasimamia uundwaji wa vyama vya ushirika imara na pia kuimarisha vyama vya ushirika vilivyopo. Tambueni kuwa kuwepo kwa ushirika imara ni njia muhimu ya kutatua changamoto nyingi zilizopo zama hizi,” alisema.
Alisema katika mwaka 2021/2022 vituo vya kukusanyia maziwa 238 vilianzishwa kwenye maeneo yenye mfumo wa masoko unaounganisha viwanda vya kusindika maziwa.
Kutokana na hali hiyo, usindikaji wa maziwa katika viwanda umeongezeka kutoka lita milioni 75.9 mwaka 2020/2021 hadi lita milioni 77.6 mwaka 2021/2022.
Ongezeko hilo alisema limetokana na kuongezeka kwa uwekezaji hususani kupitia sekta binafsi katika ujenzi wa viwanda vya kusindika maziwa.