Wanafunzi 832 Iringa Vijijini hawajulikani walipo

WANAFUNZI 832 kati ya 8,089 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za sekondari Iringa Vijijini hawajaripoti katika shule walizopangiwa na hawajulikani walipo.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Verronica Kessy ametoa hadi Machi 31 mwaka huu wanafunzi hao wawe wametafutwa na kuripoti katika shule walizopangiwa.

Mbali na yeye mwenyewe kushiriki oparesheni hiyo, Kessy aliwataja wengine watakaohusika kuwasaka wanafunzi hao kuwa ni pamoja na wazazi au walezi wa watoto hao, watendaji  na wenyeviti wa vijiji na kata, madiwani,  mkurugenzi wa halmashauri na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alitoa maelekezo hayo kwenye mkutano wa wadau wa elimu wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa uliofanyika leo mjini Iringa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo watu binafsi, mashirika ya kimataifa, idara za serikali, kampuni na taasisi za fedha.

Katika mkutano huo, wadau hao waliazimia pia kuanzisha ujenzi wa mabweni ya wanafunzi hususani wasichana katika shule zote 34 za serikali zilizopo katika halmashauri hiyo.

Aidha mkutano huo umeitaka jamii yote katika maeneo husika wakiwemo wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanakuzwa kwa kuzingatia maadili na nidhamu, ili kukilinda kizazi kilichopo na kijacho dhidi ya tishio kubwa la vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, ulawiti pamoja na vitendo vya ushoga na usagaji.

Mengine yaliyoazimiwa ni pamoja na kuendeleza kampeni ya utoaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wote wa shule za kutwa itakayohusisha michango ya wazazi au walezi, huku walimu wakihimizwa kufundisha kwa bidii.

Akitoa tathmini ya mwenendo wa elimu, Ofisa Elimu Sekondari wa halmashauri hiyo, Sylvester Mwenekitete alisema hali ya ufaulu mitihani ya kidato cha pili na cha nne inazidi kuimarika katika halmashauri yake yenye shule za sekondari 49, ambazo kati yake 34 ni za serikali.

“Tunapata mafanikio makubwa sana katika sekta hii ya elimu. Tunaona ufaulu unaongezeka mwaka hadi mwaka katika shule zetu nyingi.

“Na kwa zile ambazo bado ziko nyuma tunahitaji mikakati ya pamoja ili kuziinua,” alisema na kutoa takwimu hizo za ufaulu.

Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa aliwapongeza watumishi wa halmashauri yake kwa jinsi wanavyosimamia vyema sekta hiyo, akisema wanastahili pongezi na kuungwa mkono.

 

Habari Zifananazo

Back to top button