Wanafunzi Geita wapewa vitabu 52,683
SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha kupigania haki na usawa wa watoto na wasichana, Plan International tawi la Geita, limejitolea vitabu 52,683, kwa wanafunzi wa shule za msingi mkoani Geita.
Makabidhiano ya vitabu kati ya Plan International na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita yamefanyika Shule ya Msingi Mkoani, ambapo kuna vitabu ya Hisabati, Sayansi, Kiswahili, Kiingereza na vitabu vya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mradi Shirika la Plan International, Nicodemus Gachu, amesema hayo na kufafanua kati ya vitabu vilivyotolewa, vitabu 43,800 vimenunuliwa kupitia mradi wa Kuwezesha Wasichana Balehe Kuendelea na Masomo (KAGIS).
Amesema mradi wa KAGIS unafadhiliwa na serikali ya Canada, huku vitabu 8,883 vimenunuliwa kupitia mradi mwingine ,ambapo vitabu vyote vimegharimu kiasi cha Sh 438,289,448, lengo likiwa ni kufanikisha upatikanaji sawa wa elimu ya msingi.
“Mradi huu (KAGIS) unatekelezwa katika mkoa wa Geita na lakini pia katika mkoa wa Kigoma, ukiwa unalenga kuwafikia jumla ya watoto 102,336 na unatekelezwa kwa miaka mitano na utekelezaji wake umeanza toka mwaka 2021,” amesema.
Mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Mkoani, Loyce Andrea, amesema vitabu hivo hasa vya masomo ya sayansi vitaongeza chachu kwao kufanya vizuri zaidi kuelekea mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amepongeza hatua hiyo na kusisitiza jamii kuendelea kuunga mkono juhudi za kuwekeza kwa watoto wa kike, ili kufikia azma ya kuleta mapinduzi na usawa katika taaluma na nyanja za uongozi.