Wanafunzi Kasulu waomba kutekelezwa sheria dhidi ya ukatili
WANAFUNZI wa shule za sekondari wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameitaka serikali na wadau wa kupinga ukatili kusimamia kikamilifu utekeleza wa sheria za adhabu kwa wabakaji na wanaowapa mimba wanafunzi ili kutokomeza vitendo hivyo.
Wakizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwenye kijiji cha Makere wilayani hapa wanafunzi hao wamesema kuwa licha ya kuwepo kwa adhabu kubwa ya kifungo kwa wabakaji na wanaowapa mimba wanafunzi bado watu wengi wanafanya na hawapati adhabu kulingana na makosa.
Mmoja wa wanafunzi hao, Judith Masatu Mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Makere alisema kuwa adhabu kwa wakosaji zipo lakini utekelezaji ake unalega lega hali ambayo inafanya watu wengu kutoogopa kujihusisha na makosa hayo.
Kwa upande wake mwanafunzi, Maria Samwel mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Makere Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma alisema kuwa bado hatua hazijachukuliwa kwa wanaowapa mimba wanafunzi kwani inapotokea kitendo hicho wanawajua lakini wanapopelekwa polisi muda mchache wanatoka na kuwaona wakiendelea kuranda mitaani wakati wanafunzi wanafukuzwa shule.
Akizungumzia changamoto hiyo katika kilele cha maadhimisho hayo, mwezeshaji kutoka Shirika la World Vision, Francis Farayo alisema kuwa kamati za MTAKUWA za ngazi ya mitaa, kijiji hadi taifa zinalo jukumu kubwa la kusimamia kwa karibu mwenendo wa matukio ya ukatili kwa watoto na kusimamia kwa karibu katika kuchukua hatua kwa wahusika.
Farayo alisema kuwa wadau kutoka sekta binafasi wanayo nafasi katika kusaidia kutoa elimu na usaidizi mweingine kufanikisha mpango huo lakini serikali kupitia kwenye vyombo vyake vinapaswa visimame kidete kuhakikisha wakosaji wanachukuliwa hatua.
Hata hivyo alisema kuwa wazazi na jamii ni changamoto kubwa katika kuhakikisha wanasimamia kwa karibu suala la kuchukua hatua kwa wabakaji na watu wanaowapa mimba wanafunzi kwani wengi wanaharibu ushahidi ili kuwanusuru ndugu zao hivyo pamoja na kuwepo kwa sheria bado ushahidi wa kutosha wawatia hatiani watuhumiwa haupatikani.
Kwa upande wake Afisa ustawi wa jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Jalali Kiumbe alisema kuwa kwa nafasi yao kwa kushirikiana na dawati la jinsia la jeshi la polisi na wadau mbalimbali wamekuwa wakisimamia kupinga vitendo vya ukatili na kuchukua hatua lakini jamii imekuwa na changamoto kubwa katika kuharibu mwenendo wa kesi za ukatili kwa watoto.