Wanafunzi la kwanza Shule ya Mungumaji wavuka lengo

WANAFUNZI walioanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mungumaji, mwaka huu 2023 wamefika 189 sawa na zaidi ya asilimia 100 ya matarajio.

Mafanikio hayo yamesababisha changamoto za upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa na madawati.

Ili kufikia malengo ya kuwajengea wanafunzi uwezo wa kumudu K tatu (Kusoma, Kuhesabu na Kuandika), ufumbuzi wa changamoto hizoni muhimu upatikane mapema.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Charles Kirimba, anasema walimu wawili wametengwa ili wafundishe darasa hilo,  lakini mpaka  wakati akizungumza ni mwalimu mmoja aliyekuwa akifanya kazi hiyo, kwa sababu mwenzake alikuwa likizo ya kujifungua.

Mwalimu Eva Mpumbuji anayefundisha wanafunzi hao anaelezea changamoto anazokabiliana nazo kazini kuwa ni pamoja na utoro.

“Tumewagawanya katika makundi mawili, 100 wanaingia darasani saa 1: hadi saa 5 asubuhi, wengine wanaingia saa 5 asubuhi hadi saa 8 mchana,” anasema.

Mpumbuji anasema wanaoingia darasani saa 5 asubuhi wanapokutana na  wenzao waliotoka darasani muda huo, nao wanageuza, wanaarudi nyumbani.

Anasema pia ufundishaji wa mwanafunzi wa darasa la kwanza ni tofauti na madarasa mengine kwa kuwa mwalimu hutakiwa kumfikia kila mtoto, hata kumshika mkono kumsaidia kuumba herufi, jambo ambalo khaliwezekani kutokana na mazingira  yalivyo.

 

Mwalimu Eva Mpumbuji. (Picha zote na Editha Majura).

Anashauri yaongezwe madarasa matatu ili yawe manne, ili kila darasa liwe na wanafunzi 47.

Pia anashauri  walimu waongezwe wawe wanne, ili wanafunzi hao wote waingie na kutoka darasani kwa pamoja.

Anasema ikiwa hivyo utoro utakoma,  ari ya kusoma kwa watoto na hata walimu kufundisha itaongezeka.

Anabainisha uwepo wa wanafunzi wanaoishi vijiji vilivyo mbali na shule, ambao hutembea umbali wa kati ya Km tano hadi Saba na kwamba wanaotoka darasani mchana, jua linakua kali na ikumbukwe ni watoto wenye umri kati ya míaka sita na saba.

Kaimu Ofisa Elimu – Msingi wa Manispaa  Manispaa ya Singida, Beno Magesa, amesema watashirikiana na uongozi wa shule hiyo kuona jinsi watakavyopata  walimu wa kusaidiana na Mwalimu Eva, kutoka katika walimu waliopo kwenye shule hiyo,  kwa kuwa upungufu wa walimu upo kwenye manispaa nzima.

Anasema Halmashauri hiyo imetenga Sh Milioni 25 kutoka kwenye mapato yake ya ndani, kumalizia maboma mawili ya madarasa yaliyopo kwenye shule hiyo na  kwamba hata Mradi wa BOOST (Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Msingi na Awali nchini) utajenga madarasa mapya  mawili kwenye Shule hiyo.

Serikali inatekeleza Mradi wa Shule Bora, unaolenga kuboresha mazingira ya kufundisha na kufundishia katika shule za  awali na msingi kwenye mikoa tisa, Singida ukiwemo.

Mradi huo umedhaminiwa na Serikali ya Uingereza kwa Sh Bilioni 271 na utatekelezwa kwa miaka Sita, itakayofikia ukomo Mwaka 2027.

Habari Zifananazo

Back to top button