Wanafunzi sekondari kufundishwa ujasiriamali

ZAIDI ya wanafunzi 1000 kutoka shule za sekondari Mkoa wa Mwanza, wanatarajia kunufaika na elimu ya ujasiriamali kutoka Chuo Cha Elimu ya Biashara(CBE), Kampasi ya Mwanza.

Hayo yamesemwa leo na Mratibu wa klabu za ujasiriamali wa shule za sekondari Mkoa wa Mwanza kutoka CBE, Frank Katumbaku, wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo katika shule ya Sekondari Kangaye, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

‘’ Uanzishaji wa vilabu hivi vya ujasiriamali utasaidia sana katika kuondokana na tatizo la ajira nchini. Tunawaomba walimu wa shule zote Mwanza watupe ushirikiano wa kutosha,’’ amesema Katumbaku.

Amesema kwa sasa utoaji wa elimu za ujasiriamali umeanza katika Wilaya ya Ilemela na wamefanikiwa kuanzia shule tano za sekondari za Nundu, Kangaye, Nyasaka, Buswelu na Nyamanoro.

Amesema kwa sasa wameanza na wilaya ya Ilemela kutokana Ilemela ndio wilaya chuo chao kinapopatikana.

Ameahidi wakimaliza shule za sekondari Ilemela watendelea na shule za wilaya zingine za Mwanza, kisha watahamia katika mikoa mengi ya Kanda ya Ziwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa CBE, Kampasi ya Mwanza Dk Meschack Siwandeti, amesema maelekezo ya kuanzisha utoaji wa elimu ya ujasiriamali ni maelekezo ya bodi ya CBE na azma ya kutimiza lengo la Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni lazima kila kijana awezeshwe kuwa na uwezo kutafsiri changamoto katika jamii na kuwa fursa.

Alisema mafunzo hayo pia yanatolewa katika kampasi za Dar es Salaam, Lindi na Mbeya.

 

Habari Zifananazo

Back to top button