WANAFUNZI wa Ipagala jijini Dodoma wamepunguziwa mwendo baada ya serikali kukamilisha ujenzi wa Shule ya Msingi Swaswa ambayo imekuwa hitaji kubwa la wananchi kwa miaka mingi.
Akizungumza Diwani wa Kata ya Igagala Gombo Kamuli amesema ujenzi wa shule ya Msingi Swaswa ni ukombozi mkubwa kwa wanafunzi wa kata ya Ipagala eneo la Swaswa ambao walikuwa wanatembea umbali mrefu.
“Tunaishukuru serikali kutekeleza miradi ya maendeleo katika kata yetu, ujenzi wa kituo cha afya, nyumba za walimu, Barabara, visima vya maji, zoezi la upimaji maeneo yote ya mtaa, na sasa shule hii ya Swaswa.
“Pongezi za pekee zimfikie Rais wetu, Samia Suluhu Hassan na mbunge wetu Anthony Mavunde, hakika tunaweza kusema kata yetu ina bahati sana,”amesema.
Akizungumza kwa upande wake Mavunde amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kwa dhati kabisa katika kuboresha na kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi na kwamba ndani ya miezi mitatu zimejengwa shule za msingi tano katika Jiji la Dodoma, ikiwemo Shule ya Msingi Swaswa.
“Mtakumbuka kwamba mwaka 2020 mimi na Diwani Gombo tulikuja hapa kuahidi ujenzi wa Shule ya Msingi Swaswa na leo nina furaha kubwa kuiona ahadi hii imetekelezeka na kuwapunguzia mwendo mrefu watoto wa shule, ”amesema na kuongeza:
“Tunaishukuru serikali chini ya Mh.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa shule hii ambayo ni mkombozi mkubwa kwa wanafunzi wa eneo la Swaswa,”amesisitiza Mavunde
Comments are closed.