Wanafunzi wa kike kuunganishwa vyuo vya ufundi
DAR ES SALAAM: KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi (Neec), Beng’i Issa ameahidi kuwasaidia wanafunzi wa kike waliomaliza sekondari wenye uhitaji ili kujiunga na vyuo vya kiufundi.
Beng’i ameahidi hayo wakati wa hafla ya kuchangisha vifaa vya shule iliyoandaliwa na Shirika la Macho kwa Jamii mkoani Dar es Salaam, kwa watoto wenye uhitaji ili viwasaidie katika masomo yao kipindi hiki shule zinapofunguliwa.
Amesema elimu hiyo inatolewa kwa ufadhili wa serikali kwenye vyuo vya kiufundi ambavyo vipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Tutahakikisha tunawaunganisha ili hawa watoto waweze kupata elimu hiyo ya ufundi na tunaamini elimu ya ufundi ni muhimu kwa ajili ya kusaidia mtu kumpa maarifa ya kujiendeleza na kujijengea uchumi wake,” amesema.
Amesema Neec pia itawasaidia wanawake waliojitolea kuwalea watoto hao wenye mahitaji wanaoanzia miaka mitatu na kuendelea, kuwawezesha kiuchumi ili nao waweze kujikwamua.
“Tutaendelea kuwasaidia wanawake ambao wanashughulika kwenye taasisi hii ambao ni wanachama ili tuweze kuwapa pia fursa za kiuchumi,” amesema.
Amesema kitendo kinachofanywa na shirika hilo ni kitu kizuri kwa sababu watoto wengi hawana wazazi, hivyo wanatafutiwa walezi ambao wanawafuatilia watoto hao kwenye masomo yao.
Naye Wakili wa Serikali ambaye ni mdau wa shirika hilo, Kijja Luzungana amesema Macho kwa Jamii linasaidia serikali kuwafikia wananchi wake hasa waliopo katika hali ngumu katika mahitaji mbalimbali.
Amesema amekuwa akitoa mafunzo kwa jamii ili kukumbusha mambo ya msingi katika masuala ya haki za mtoto, usalama wa mtoto na kuwalinda ili wasijikute wamekinzana na sheria au kuonewa kutokana na makosa ya kijinsia au kunyanyaswa kijinsia.
“Vile vile kumsaidia mtoto kufahamu namna ya kujilinda na kufahamu haki zake na namna ya kufahamu hapa nimefanyiwa ukatili wa kijinsia ninastahili msaada wa kisheria haraka kwa kumshirikisha mzazi au mlezi na kufika katika vyombo vya sheria hata mahakamani ili kutoa ushahidi wake,” amesema.
Pia amesema amekuwa mdau wa kukuza mfuko wa shirika hilo kiushauri, kifedha na kushirikisha kikundi kilichopo karibu naye cha Ladies of Victory ambacho kilitoa mchango wao ili kuwasaidia watoto wenye mahitaji kwenda shule.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo la Macho kwa Jamii, Theresia Lihanjala amesema wapo kwa lengo la kumsaidia mtoto wa kike, pia wamejikita eneo la utetezi wa haki za mtoto wa kike.
Amesema katika kumpambania mtoto wa kike wamejikita maeneo mbalimbali likiwemo la elimu.
Amesema wanasaidia watoto yatima, wengine wana wazazi lakini wanapitia ukatili.
Amesema kwa kuwa shirika hilo halina wafadhili ndio maana wameitisha hafla hiyo ya kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto hao waweze kwenda shuleni kipindi hiki shule zinapofunguliwa.
Amesema katika harambee walioyoifanya walihitaji Sh milioni sita kwa sababu wana watoto 20 wanaosoma lakini wamepata kiasi kidogo, alitoa wito kuendelea kusaidia watoto wenye uhitaji waweze kwenda shuleni.