Wanafunzi wabuni roboti inayotabasamu darasani

DAR ES SALAAM: WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari ya Kimbiji wametengeneza Roboti ya gari inayotabasamu wakiwa darasani.

Uvumbuzi huo unaotambulika na mamlaka ya Taasisi ya Elimu nchini (TET) ni utekelezaji wa mafunzo kwa vitendo ambayo wamekuwa wakifundishwa shuleni hapo kupitia mradi wa Korea E- Learning Improvement Cooperation (KLIC)

Wanafunzi hao kupitia masomo ya fikizia na uchoraji wameweza kuonyesha umahiri wao kwa kufanya mafunzo kwa vitendo wakiwa na walimu na wanafunzi wa nchini Korea katika eneo la utengenezaji wa gari la Roboti inayotabasamu wakiwa darasani katika ziara ya wajumbe kutoka Korea Kusini.

Mwakilishi wa walimu waliopo kwenye ziara hiyo kutoka nchini Korea Kusini, Kim Chi Gon amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wanakuza utumiaji wa TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji hapa nchini na kwamba kwa sasa ulimwengu umebadilika hasa katika eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Kupitia mradi huo wa Korea E- Learning Improvement Cooperation (KLIC) shule nne nchi zimenufaika ambazo ni shule za msingi Tegeta A, Mabatini na Shule za Sekondari za Kimbiji na Mkombozi ya Njombe

Aidha, akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Utafiti,Habari na Machapisho wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Kwangu Masalu amewaasa wanafunzi na walimu wa shule hizo zinazonufaika na mradi kutunza vifaa walivyopatiwa ili viweze kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi katika eneo la TEHAMA ambako dunia ndiko inakoelekea.

Mradi huo upo chini ya ofisi ya elimu ya Gwangju Metropolitan ya nchini Korea ya Kusini, wenye lengo la kuboresha elimu nchini katika eneo la TEHAMA,

Katika ziara hiyo, wajumbe wa Korea wametoa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kujifunzia masomo kwa vitendo na kutoa elimu ya namna ya kuvitumia kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo .

Nae, Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kigamboni Twidike Ntima ameshukuru kwa shule hiyo kupatiwa vifaa vya TEHAMA ambapo imesaidia walimu kufanya kazi kwa urahisi.

Amesema iwapo mradi huo utapelekwa shule zote za Tanzania itasaidia wanafunzi wengi na walimu kupiga hatua katika masuala ya elimu hususani TEHAMA.

Kwa upande wa Mkuu wa shule hiyo Joyce Ndaona amesema kwa sasa walimu wa shule hiyo wamepata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa nchini Korea ya Kusini ambapo wameweza kupata ujuzi wa kurahisishiwa kazi hasa katika eneo la ufundishaji na kuwapa nafuu wanafunzi kutumia TEHAMA kwenye ujifunzaji tofauti na awali.

Habari Zifananazo

Back to top button