Wanafunzi waishukuru serikali kufundishwa Tehama

WANAFUNZI wameshukuru kuwekewa maabara yenye kompyuta zinazowawezesha kujifunza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Wanafunzi hao ni kutoka Shule ya Sekondari Samia Suluhu Hassan na shule ya msingi Samia waliohamia kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Wanafunzi hao zaidi ya 694 walitoka Ngorongoro kwenda Msomera wakiwamo wavulana ni 353 na wasichana 341.

Wenzao 189 kutoka shule zinazowazunguka za Msomera, Mainga na shule nyingine walisema compyuta za kisasa walizofungiwa shuleni zinawapa fursa ya kujifunza vizuri.

Wazazi na walezi wao waliotangulia kuhama kwa hiyari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera.

Wanafunzi Naingia Kea na Mathayo Laizer wanaosoma shule ya Msingi Samia Suluhu Hassan walisema wanajivunia kusoma kwa uhuru.

Waliishukuru serikali kuwatoa Ngorongoro kwenda Msomera kwani awali wakiwa Ngorongoro walikuwa wakikumbana na baridi kali ikiwemo wanyama wakali.

Walisema hali hiyo ilihatarisha usalama wa maisha yao lakini walipofika Msomera, wameona mwanga zaidi katika elimu kwani wamejengewa shule zenye madarasa na madawati likiwemo darasa maalumu la kompyuta lenye vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwaongezea uwelewa katika masomo yao.

“Ngorongoro tulikuwa tunatembea umbali mrefu lakini hapa Msomera tunatembea umbali mfupi sana na tunafundishwa vema na walimu wetu kwenye masomo yetu lakini kikubwa zaidi ni hizi kompyuta za kisasa ambazo kule Ngorongoro hatukuwahi kuziona mashuleni,” alisema Naingia.

Laizer alisema kuwa yeye na wanafunzi wenzake walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita tano kufuata elimu kwenda na kurudi huku wakiwa wamevaa masweta kujikinga na baridi kali lakini tangu walipofika Msomera, hivi sasa wanavaa sare za shule bila hata kuvaa masweta na kufika shule kwa haraka sababu umbali umeisha na hata utulivu wa kusikiliza masomo upo kutokana na mazingira rafiki kwao.

Wakati huo huo, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Charles Andrea alisema shule hiyo ni miongoni mwa shule zilizopokea wanafunzi waliotokea wilayani Ngorongoro kuja Msomera yenye madarasa zaidi ya saba ikiwemo miundombinu ya kompyuta ikiwemo kufungwa mkongo wa taifa wa mawasilino na vifaa vya kisasa vya teknolojia

Alisema awali shule hiyo ilianza na wanafunzi 210, badaye wakawa 470 ambapo hadi sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 888 wa darasa la kwanza hadi la saba ambapo kati yao wavulana ni 429 na wasichana ni 459.

Alisema watoto 694 waliotokea Ngorongoro ikiwa wavulana ni 353 na wasichana 341 huku wanafunzi 189 wakitoka katika shule mbalimbali zinazowazunguka ambazo ni Msomera na Mainga na shule nyingine.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Msomera, Mwalimu Mary Msue alisema shule hiyo ipo Kata ya Misima yenye jumla ya wanafunzi 203.

Alisema shule hiyo ilianza mwaka jana ikiwa na wanafunzi 16 na badaye idadi ya wanafunzi iliongezeka zaidi na uelewa wao ni mzuri lakini pia wanatumia kompyuta kuwafundishia masuala ya Tehama.

Alisema kompyuta zinawarahishia kazi kwani wanafunzi wanajifunza kwa vitendo yakiwamo masomo ya sayansi.

Habari Zifananazo

Back to top button