WANAFUNZI wa shule za msingi za kata ya Nzihi wilayani Iringa wameitaka serikali na wadau wao wote wa maendeleo kuwasikiliza na kuwashirikisha katika maamuzi mbalimbali yanayohusu maisha na maendeleo yao.
Katika risala yao iliyosomwa na Ayuni Ngwale katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Kidamali, wanafunzi hao walizungumzia pia changamoto ya lishe inayowakabili baadhi yao na jinsi inavyoathiri ukuaji wa miili yao na kudumaza akili.
Aidha wanafunzi hao wamezungumzia ongezeko la watoto wanaotumia mitandao ikiwemo ya simu bila idhini na usimamizi wa walezi au wazazi na jinsi wanavyokutana na unyanyasaji na ukatili ukiwemo wa kingono.
“Katika mitandao hiyo tunapokea maoni mabaya hususani kuhusu miili yetu huku tukikumbana na matusi, unyanyasaji wa kingono na kuchekwa maumbile yetu kupitia jumbe fupi, picha chafu na video,”alisema Ngwale.
Ngwale aliwaomba watanzania kuzingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu huu wa kidigitali na kuungana kutokomeza ukatili dhidi yao.
Katika kukabiliana na changamoto ya lishe kwa wanafunzi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa alisema halmashauri yake imeweka azimio kwa shule zote za msingi na sekondari kutoa mlo wa mchana kwa wanafunzi wake wote kupitia chakula kitakachochangwa na wazazi au walezi wao.
“Kipindi hiki ni cha mavuno, sisi tumeweka mkakati wa kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa wazazi ambao mpaka itakapofika Juni 30 mwaka huu watakuwa wameshindwa kupelekea chakula katika shule ambazo watoto wao wanasoma,” alisema.
Alisema lishe bora ni haki ya mtoto kama zilivyo haki zingine za msingi kama elimu, afya, malazi na malezi bora na kwamba haki hizo zinapaswa kulindwa kwa nguvu zote.
Mhapa alisema halmashauri yake inatambua kwamba mwanafunzi anapokosa chakula shuleni anaweza kupata madhara ikiwemo kukosa usikivu wakati wa kujifunza, mahudhurio hafifu na hata kukatisha masomo ndio maana imeweka lazima kwa shule zote kutoa mlo wa mchana.
Alisema lazima hiyo ni utekelezaji wa mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi na akawataka wazazi na walezi wote wa watoto hao kuuunga mkono mwongozo huo.
Kwa upande Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii ya wilaya hiyo, Swaum Kweka alizungumzia sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 pamoja na mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa yanayohusu haki za mtoto.
Kweka alisema katika kuzingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidigitali halmashauri yao inatambua changamoto zinazolikabili kundi hilo na katika kukabiliana nazo imeendelea kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao, kuwasikiliza na kuyafanyia kazi mambo yanayoharibu maisha yao.
“Lakini tumeunda majukwaa ya wanawake katika kata zote na hatua ya pili ni kuyaunda katika ngazi za vijiji ili yatumike kikamilifu kushughulikia changamoto zinazowahusu wanawake na watoto vikiwemo vitendo mbalimbali vya ukatili dhidi yao,” alisema.