Wanafunzi wapatiwa elimu ya afya

BAADHI ya wanafunzi wa sekondari katika kata tatu Wilaya ya mtwara mkoani Mtwara wamepatiwa elimu ya hedhi salama kwa mtoto wa kike itayowasiaidia kutambua haki yao ya afya, kuondokana na changamoto ya kushindwa kuhudhuria baadhi ya vipindi darasani.

Kata hizo ni Nanyamba, Ndumbwe pamoja na Nyundo.

Akizungumza jana wilayani humo wakati wa mafunzo hayo ya siku moja, Meneja Mradi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii nchini la Smile for Community Aneth Kiyao amesema wameguswa kutoa elimu hiyo ili kuwawesha watoto wa kike  kujitatambua na kufamu haki yao ya afya.

Advertisement

‘’Elimu hii itasaidia mabinti kupata uelewa kuhusu hedhi salama pia tumewapatia taulo za kike ili kuwawezesha waweze kuhudhuria vipindi vyote darasani bila kukosa kwasababu baadhi ya wazazi wanashindwa kumudu gharama ya hizi taulo kutokana na mazingira hivyo kumfanya binti ashindwe kuhudhuria baadhi ya vipindi darasani’’,amesema Kiyao

Ameongeza kuwa, ‘’Kupitia hizi taulo zitamfanya awe na amani mda wote awazii tena mazingira ya hedhi kama mwanzo atahudhuria vipindi  vyote darasani bila kukosa na suala la kushindwa kuhudhuria baadhi ya vipindi anakuwa anawaza sana mazingira na kukosa amani kwahiyo anashindwa kuja shule mpaka amalize siku zake’’amesema

Shirika hilo la Smile for Community linatekeleza mradi huo kwa ufadhili wa shirika lisilo la (Legal Services Facility) unaotekelezwa kipindi cha pili cha mradi ndani ya miezi sita kuanzia Juni mpaka Novemba 2023 ambapo awali ulianza kutekelezwa kwa miezi minne Novemba 2022 mpaka Februari mwaka huu.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Nyundo wilayani humo Agnes Kinyaiya amesema kila mwezi watoto  watano mpaka sita wanakosa vipindi darasani kutokana na changamoto hiyo ikizingatiwa baadhi yao wanaishi mbali kidogo na shule ‘’Kupitia hizi pedi ule utoro utapungua mana watoto wapo waliyotoka katika familia duni hivyo wakati mwingine wanashindwa kumudu hizi pedi za dukani kwahiyo tunashukuru na tunaomba hili zoezi liwe endelevu’’

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Ndembwe wilayani humo, Bishala Salumu alisema kitendo cha shirika hilo kujali na kuona umuhimu wa kuwapatiwa elimu na taulo hizo ni msaada mkubwa kwao kwasababu sasa watasoma kwa amani na bila kukosa vipindi darasani.

 

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *