“Wanahabari tumieni vizuri kalamu zenu”

LINDI: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka waandishi wa habari nchini kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, weledi na maadili ya tasnia ya habari sambamba na kutoa kipaumbele kwa habari sahihi, zenye tija, zinazo chochea maendeleo na maslahi kwa umma.
Ameagiza hayo leo akiwa mkoani Lindi katika Mkutano Mkuu wa Saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kuwataka waandishi wa habari kuzingatia sheria za nchi, pia kuchukua tahadhari za usalama katika utendaji wa shughuli zao za kila siku.
“Unaweza kuwa na kitambulisho alafu mbele kuna shimo. Usiingie kwenye shimo kwakuwa una kitambulisho,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, kiongozi huyo ametoa wito kwa wananchi kutowabughudhi wala kuwashambulia wanahabari wanapotenda majukumu yao ya kila siku.
“Kushambulia wanahabari ni uhalifu kama uhalifu mwingine.” Amesema kiongozi huyo.
Aidha, mkuu huyo amesema waandishi wa habari wapo kisheria na Serikali inawatambua, hivyo wananchi na waandishi kwa pamoja wawe watiifu wa sheria. Ukikiuka utadhibitiwa.
Akizungumzia kuelekea maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025, amewataka waandishi wa habari kutangaliza nchi mbele kwa kuandika habari za misingi, uzalendo na maslahi ya umma.
1 comments

Comments are closed.