DSM; UKOSEFU wa mikataba ya ajira, kipato duni imetajwa kuwa blanketi zito lililofunika tasnia ya habari na kuchochea rushwa ya ngono ndani ya vyombo vya habari.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam, katika kikao cha majadiliano kilichoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T) kupitia mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari wanawake, ambapo Wanahabari wanawake wametakiwa kujiamini, kujituma katika kazi, kujitambua ili kuepuka kuingia kwenye mitego ya rushwa ya ngono.
Akizungumza Ofisa Uchechemuzi kutoka Tamwa, Florence Majani amesema; “Tasnia ya Habari ni muhimili wa nne wa dola, lakini kuna muda tunajiuliza hivi labda kada ya madaktari au wanasheria walipaswa kuwa muhimili wa nne wa dola?
“Tasnia ya habari inadharaulika si chochote kwa mtu yoyote kutokana na mazingira yanayotuzunguka,” amesema Florence na kuongeza:
“Asilimia kubwa hawana mikataba ya kudumu ya ajira, kipato kidogo, ndio maana hakuna anayetaka mwanae aje arithi kazi hii, tasnia ya habari imekuwa ni mshumaa unaomulika wengine huku yenyewe inateketea,” amesema.