Wanahabari watakiwa wasichonganishe serikali na wananchi

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kutumia mafunzo ya umahiri wa uandishi wa habari wanayoyapata kuleta mchango wa maendeleo na ustawi bora kwa taifa.

Aidha, wametakiwa wasitumie mafunzo hayo kuigombanisha serikali na wananchi wake.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alisema hayo akifunga mafunzo ya siku nne ya uandishi wa habari za uchunguzi kwa waandishi wa habari wanawake yaliyofanyika mkoani Kigoma kwa uratibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Waandishi wa habari wanawake kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania ambao walishiriki mafunzo ya uandishi wa habari za uchunguzi yaliyofanyika mkoani Kigoma kwa uratibu wa Baraza la habari Tanzania (MCT) . (Picha na Fadhili Abdallah)

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Ester Mahawe alisema uandishi wa habari za uchunguzi unaozingatia uzalendo na maadili ya taaluma hiyo una manufaa makubwa kwa maendeleo ya taifa na ustawi kwa watu wake.

Awali Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema mafunzo hayo ya siku nne kwa waandishi wa habari wanawake 17 kutoka Tanzania Bara yamelenga kujenga uwezo kwa waandishi hao kufanya habari na makala ambazo zinaelezwa kuwa haziwezi kufanywa na wanawake.

Alisema kuwa chini ya Mkufunzi wa mafunzo hayo, Laurence Kilimwiko, waandishi wa habari hao wanawake wanajengewa uwezo wa kuibua na kwenda kufanya habari na makala zilizofanyiwa uchunguzi wa kina kuondokana na habari za uchunguzi wa kawaida.

Habari Zifananazo

Back to top button