NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete ameagiza wananchi 949 kati ya 1,405 waliopo Mji Mpya Kata ya Mabwepande Dar es Salaam, ambao hawajafanya utaratibu wa malipo katika viwanja walivyopewa na serikali ili wapate hati, wafanye hivyo wawe wamiliki halali.
Ridhiwani alisema hayo baada ya kupata malalamiko toka kwa wananchi hao kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeshindwa kutekeleza agizo la serikali la kuwapatia hati.
Alisema serikali ilitoa eneo bure kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko mwaka 2011, hivyo ni juu yao kulipia maeneo yao ili wapewe hati zao kwani inawezekana wakati wanakabidhiwa kuna jambo hawakulielewa vizuri.
Alisema mpaka sasa wananchi 456 wameshapata hati zao baada ya kukamilisha mchakato wa kulipia, bado 949 kati ya 1,405 waliohamia eneo hilo. “Serikali ilitwaa maeneo ikagawia ardhi wananchi, zipo gharama za kisheria za kumiliki ardhi. Ili upate hati za umiliki inabidi uende ardhi ulipe nwenyewe,” alisema.
Pia alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria za ardhi ya mipango miji mtu yeyote anayekaa eneo lililopangwa anatakiwa ndani ya miaka mitatu awe ameliendeleza. Alifafanua kuwa toka mwaka 2011 bado haujafanyika utaratibu wa kuwanyang’anya hivyo jambo hilo haliwapi uhakika kuwa hilo eneo wanakaa nalo milele.
Ridhiwani alitoa ufafanuzi huo ikiwa ni miaka 11 sasa kwa wakazi 604 walioitii serikali na kuondoka kwa hiari maeneo hatarishi ya mabondeni Dar es Salaam, kupelekwa Mtaa wa Mji Mpya, Kata ya Mabwepande. Watu hao walieleza kuwa bado hawajapewa hati zao kama ilivyoelekezwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwa wakati huo.
Pia Naibu Waziri huyo alisema wakati wananchi wanapewa maeneo hayo, Rais Jakaya Kikwete alielekeza wawekewe zuio la kutouza ardhi kwa miaka 25.
“Bila shaka watu wengi wameuza maeneo lakini ni ngumu kubadili mmiliki kutokana na hilo,” alisema.
Wananchi hao 604 walisema baada ya wao kuondoka kwa hiari kuitii serikali walipewa ahadi hiyo tofauti na wengine waliofuata baadaye baada ya kuomba kupatiwa maeneo hayo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mji Mpya, Mohammed Basta alisema hayo alipozungumza na HabariLEO kuhusu miaka 11 ya maisha mapya ya wakazi hao 604 tokea walipohamia Mji Mpya mwaka 2011.
Uchunguzi uliofanywa na HabariLEO umebaini kuwa wananchi waliohama kutoka Kata za Mchikichini eneo la Mafuso, Kata ya Upanga mtaa wa Charambe Minazini, mtaa wa Suna, Hananasif, Ulongoni Ving’ung’uti, Msimbazi bondeni, Tabata, Kinyerezi na Mbagala wengi wao bado hawana hati za maeneo yao.
Hata hivyo, wale wenye uwezo ambao walilipia Sh 166,000 na kuendelea kutokana na ukubwa wa eneo ndio wenye hati.
Mkazi wa eneo hilo, Kassim Ng’wambo aliishukuru serikali kwa kuwatoa maeneo hatarishi na kuwapeleka eneo hilo ambalo kwa kaya hizo 604 kila moja ilipewa mifuko 100 ya saruji na Rais Mstaafu Kikwete, mabati manne, mbao sita na matofali 36 kutoka kwa wadau wengine. Naye Sada Msombe alisema miaka hiyo 11 katika mtaa wa Mji Mpya una mafanikio na changamoto pia.
“Tunamwombea Kikwete kwa kututoa sehemu hatarishi na kutuleta sehemu salama. Tunamshukuru Mungu mno Mungu alimpa roho ya huruma, alijua sisi ni wananchi wake, wapigakura wake na Watanzania wenzake,” alisema.
Alikiri sasa hivi eneo hilo lina shule, kituo cha polisi na hospitali kubwa inayoendelea kujengwa. “Changamoto tuliyonayo hatuna usafiri kwani huu Mji ulipangwa kitaalamu, lakini leo ukija hata ule utaalamu uliokuwa umepangwa utaonekana mainjinia hawakufanya kazi. “Tuliambiwa tutaboreshewa hizi barabara za mitaa, ambazo ilielezwa ingekuwa kama eneo la Ilala au Magomeni Mapipa,” alisema.
Mkazi Mwingine, Ramadhan Salim alisema ili kuweza kupambana kuboresha eneo lake aliuza mifuko 50 ya simenti akanunua mchanga, matofali na kupata hela ya kumlipa fundi.
Naye Gason Dutiwa alisema baada ya kuona hakuna msaada wa kupewa hati zao, alilipia na kupewa lakini changamoto iliyopo ni kwamba hati hizo zina kizuizi mtu hawezi kukopa benki wala kuweka dhamana yeyote hadi muda wa miaka 25 upite.
Comments are closed.