Wanakijiji walalamikia kutumia maji ya madimbwi

WAKAZI wa vijiji vya Butini na Kidanda, Kata ya Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamelalamikia kukosa huduma ya maji safi na salama na kulazimika kutumia maji ya kwenye madimbwi.

Wakizungumza na HabariLEO jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kidanda, Regina Mapuli na Hussein Mikidoli walisema inawalazimu  wachangie maji na wanyama.

Mapuli alisema muda mrefu kilio chao bado hakijapatiwa ufumbuzi na wanaendelea kuhangaika kutafuta maji safi na salama kipindi cha kiangazi wakati mito na baadhi ya madimbwi yanakuwa yamekauka.

“Jamani maji ni shida kipindi cha kiangazi hata hizi nguo nyeupe unazoziona hatuvai maana maji ya kufulia ni changamoto, tunaiomba serikali na sisi itukumbuke tuletewe maji ya Ziwa Victoria,” alisema Mapuli.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidanda, Shija Kaza alisema kwa muda mrefu wananchi wanakabiliwa na kukosa huduma ya maji kwani maji wanayotumia ni kutoka kwenye madimbwi na visima vya asili.

Diwani wa Kata ya Itwangi, Sonya Jilala alikiri kuwepo changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama na kilio hicho cha wananchi ameshakifikisha mamlaka husika.

“Bajeti iliyopo ni kupeleka maji vijiji vya Itwangi na Zobogo kwa mwaka huu na kuwaomba wananchi kuwa na uvumilivu wakati taratibu zingine zikiendelea,” alisema Sonya.

Kaimu Meneja wa Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Wilaya ya Shinyanga, Emaeli Nkopi alisema Kata ya Itwangi ina vijiji vinne ambapo vijiji viwili viko kwenye mradi wa maji ya Ziwa Victoria.

Nkopi alisema vijiji viwili vya Kidanda na Butini vipo kwenye maandalizi ya mradi na wanafanya usanifu ili kujua gharama za miradi na kujua chanzo watakachokitumia na kazi inatarajia kuanza mwezi huu.

Habari Zifananazo

Back to top button