Wanakijiji walia na viwavijeshi
WANANCHI wa Kijiji cha Kimange wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani wameiomba serikali kuwapatia dawa za kudhibiti wadudu aina ya viwavijeshi vamizi waliovamia mashamba yao hususani ya mahindi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimange, Said Bakari alipotembelewa na watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa mkoani Morogoro kujionea hali halisi ya tatizo hilo.
Bakari alisema wadudu hao ambao katika kijiji hicho wanawaita sondo, wamekuwa wakiwasumbua. Alisema wenye uwezo wamekuwa wakinunua dawa na kupuliza huku wasiokuwa nao wakiwaacha waendelee kushambulia.
“Mwaka jana imesababisha njaa mpaka sasa hivi watu wana njaa kwa sababu ya huyu mdudu sondo, alishambulia sana. Kwa sasa kuna mashamba yameathiriwa sasa yule mwenye uwezo kidogo ndio anawadhibiti, wale ambao uwezo wao mdogo ndio tunatoka patupu,” alisema.
Alisema pembejeo zingekuwa karibu, ingekuwa rahisi mkulima anapoona dalili za wadudu hao anadhibiti mapema. Mkulima Juma Ngowe alisema kila siku anapokagua shamba anakuta wadudu hao ambao wanasababisha uharibifu mkubwa.
Mratibu wa Utafiti, Kilimo na Ubunifu kutoka Tari Ilonga, Meshack Makenge alisema wamefika katika kijiji hicho kuangalia ukubwa wa tatizo waweze kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na viwavijeshi vamizi hao, kwa kuwa ili kumdhibiti, elimu ya kumtambua inahitajika.
“Inatakiwa elimu kuelimisha wananchi namna ya kupambana naye hususani kiasi cha kupiga dawa, kiasi cha maji na muda wa kupiga dawa. Hicho kitu ni muhimu sana,” alisema na kuongeza kuwa pia wanatoa elimu ya kumtambua mdudu huyo.
Alisema zikitumika dawa sahihi na viwango sahihi vya kuchanganya maji na muda wa kuipiga inakuwa rahisi kumdhibiti. Alisema kanuni bora zikifuatwa mkulima anapata mazao mengi katika shamba la hekta moja, kwani atapanda mimea 4,444, gunzi la mahindi linakuwa na mistari 14 na punje zake 52, matokeo yake mkulima atapata faida ya kutosha.
Mratibu za zao la Mahindi Kitaifa kutoka Tari Ilonga, Dk Arnod Mushongi ambaye naye alifika katika kijiji hicho kuangalia hali halisi ya ukubwa wa tatizo, alisema kikubwa kinachotakiwa ni maofisa ugani kushirikiana na wakulima kubaini tatizo mapema.
Alisema alichokiona ni kwamba tatizo linakuwa kubwa kutokana na wakulima kukosa elimu ya kufuata kanuni za kilimo bora na elimu ya kumtambua na kumdhibiti mapema mdudu huyo hatari kwa mazao. “Mdudu huyu ana uwezo mkubwa sana.
Anaweza kwenda kilometa 2,000, kutaga mayai zaidi ya 1,000, kujibadili na kujificha asionekane, pia ana mbinu nyingi za kumfanya aweze kuishi. Mdudu huyu anaweza kusababisha mkulima asipate mavuno kabisa au akasababisha mahindi yakaoza na kutengeneza sumu,” alisema.