ZAIDI ya wakazi 1000 wa kijiji cha Ogutu, Kata ya Naberera Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara, wameleza kupoteza imani na serikali ya mtaa wakieleza kuzuiwa kulima mazao katika mashamba yao ya siku zote.
Wakizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro katika kijiji hicho,ambao hata hivyo haukumaliza baada ya wananchi wao kumueleza kiongozi huyo kuwa tatizo kubwa ni uongozi wa kijiji hicho ambao unachangia kuwepo kwa migogoro ya umiliki wa mashamba.
Wananchi hao walisikitika kuwa licha ya uhaba wa chakula kuathiri eneo hilo, ni miaka mine sasa tangu kuzuiwa kulima katika sehemu ya ardhi iliyotengwa kwa ajili ya kilimo na serikali ya kijiji kwa utaratibu imepelekea watoto wao kushindwa kuhimili masomo kutokana na familia zao kukosa chakula.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota ambaye amefika katika mkutano huo ambao hata hivyo haukumaliza baada ya wananchi hao kumueleza kuwa hawawezi kutoa malalamiko yao akiwa na viongozi hao wa kijiji ambao wanawatuhumu kuwa ndio chanzo cha kuleta migogoro katika kijiji hicho .
Makota amesema wananchi wa hapa wamekuwa na malalamiko kwa muda mrefu na viongozi mbalimbali wamekuwa wakifika kutatua kero lakini kero hiyo imeshindwa kutatulika.
“Kuna maeneo ya malisho na maeneo ya Kilimo, sasa kuna mwananchi waliuziwa katika maeneo ya malisho lakini serikali huko nyuma ilichukua hatua ya kumsimasisha kazi mwenyekiti wa kijiji na hiyo kutokana na kubaini matatizo yaliyojitokeza katika uongozi wake lakini pamoja na serikali ya kijiji kukosea tuna haki ya kuwasikiliza wananchi ili kuona namna ya kumaliza migogoro hiyo,”. alisema Makota.
Amesema walijipanga kusikiliza mwananchi mmoja mmoja lakini zoezi halikukamilika kwani wananchi hao walisema hawana Imani na serikali ya kijiji na kuomba kuwepo kwa uchaguzi kuchagua viongozi wapya.
“Kero hii ya wananchi kudai viongozi wa kijiji walio madarakani sio wa kuchaguliwa nimeichukua na nitaifikisha TAMISEMI ili wao ndio watapanga na kuamua suala la uchaguzi,”Amesema Makota.
Kwa upande wake Mwenyekiti aliyeondolewa madarakani, Richard Meshuku amesema alitenguliwa kwa tuhuma ambazo hajazipata wala kuziewlewa na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro bila barua ila walimsimamisha na kuteuwa watu wao ambao ndio wamekuwa chanzo cha migogoro kwa wanakijiji.
“Ni miaka miwili sasa nimeenguliwa na sababu matwaka niliyokataa ni kuhusu kunyima watu kilimo kwani kuna eneo la kilimo lina muda mrefu tangu namaliza shule ya msingi nililikuta likifanyiwa kazi na wananchi bila mgogoro wowote wa wakulima na wafugaji ,”amefafanua Meshuku.
Amesema tatizo la kuzuia watu kulima ndio walilikataa kwani limekuwa likifanyika bila kushirikisha wananchi na kwenda kinyume na mikutano ya kijiji ambayo walikaa na wanakijiji kujua maeneo yapi ya malisho na kilimo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ,mmoja wa wanakijiji hao aliyefahamika kwa jina la Ramadhan Nassari ambaye amesema amepewa kiwanja cha kulima tangu mwaka 1998 na kueleza ni miaka minne sasa tangu alipokataliwa kulima katika eneo lake alilopewa kihalali.
“Tunaambiwa kwamba haya yanapaswa kuwa maeneo ya malisho, sio mashamba,” amesema Nassari na kuongeza kuwa wana hati rasmi zinazowapa haki ya kulima katika eneo hilo na walikuwa wamekuwa wakilima miaka ya nyuma bila migogoro.
Aidha wanakijiji hao wamedai kuwa wamekuwa wakilazimishwa kutoa fedha ili waruhusiwe kulima mazao japo kwa muda.
Naye Frank Mollel mwanakijiji amesema asilimia kubwa ya watu wanateseka kutokana na kuzuiwa kulima Kwa miaka minne sasa wakilima mifugo inaletwa katika maeneo ya kilimo na kufanya uharibifu na kupelekea mazao kuharibiwa na sehemu za malisho zipo na zilipitishwa na serikali ya kijiji zikianisha maeneo ya kilimo na malisho .
Naye Magreth Mariki, ambaye ni mjumbe wa zamani wa serikali ya kijiji amesema tatizo ni kwamba kuna baadhi ya wawekezaji wanataka kununua ardhi ya kijiji ndiyo maana wananchi wananyanyaswa kuhama katika maeneo yao.
“Kwa kawaida tunakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi kwa vitisho, tunamwomba Rais Samia Suluhu aingilie kati suala hili na kutusaidia kupata haki yetu kwani tumekuwa tukitesekaa na njaa watoto wetu wanashindwa hata kwenda shule.,” ameongeza Mariki.