Wananchi Bureza mambo safi huduma ya maji

WANANCHI zaidi ya 4,570 kata ya Bureza Wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera wameondokana na changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

Hatua hiyo ni baada ya Mwenge wa Uhuru kuzindua mradi wa maji Butembo wenye thamani ya Sh milioni 986.

Baadhi ya Wananchi wa kata hiyo wamesema kabla ya mradi huo walikuwa wakitumia zaidi ya saa 4 kwenda mtoni kuchota maji na wakifika wanakutana na foleni ambapo wakati mwingine walikuwa wananunua ndoo ya maji kwa Sh 500 hadi 1,000 wakati wa kiangazi.

Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Bureza, Shubira Alex alisema kutokana na changamoto ya maji katika kijiji hicho hata msichana kuolewa eneo hilo aliona kama adhabu na pengine hata familia ilidiriki kumtamkia kuwa amekosa maadili.

“Zamani wasichana kama ulimkosea mzazi alitamka kabisaa kuwa wewe nitakuozesha Bureza au Butembo ili adhabu yako iwe kuamka mapema kupanda milima ukitafuta maji na kweli hiyo kwakweli kwetu ilikuwa changamoto hasa sisi akina mama wenye familia haikuwa kazi rahisi.”Alisema Alex

Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Muleba, Mhandisi Patrice Jerome alisema mradi ni mahususi kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya maji kijiji hapo na kuwa mradi huo umetekelezwa na kampuni ya LUCOMONS LTD ya jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa mradi huo adi kukamilika umesimamiwa na mamlaka hiyo ambapo kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya mtambo wa maji, uzio, ufungaji wa pampu 2 za maji zenye uwezo wa mita za ujazo 16.9m ,ujenzi wa vituo 22 vya kuchotea maji pamoja na uchimbaji wa mitaro ya maji.

Akizindua mradi huo kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim aliipongeza serikali kwa kuendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wake na kuwataka wananchi kuendelea kuilinda miradi hiyo.

Amewapongea Ruwasa Wila ya Muleba kwa kusimamia utekelezaji wa mradi na kuwa thamani ya fedha inaonekana kwa macho.

Mwenge wa uhuru ukiwa wilayani Muleba umekagua ,kuzindua na kutembelea jumla ya miradi minane ya maendeleo.

Habari Zifananazo

Back to top button