Wananchi Chitandi waishukuru serikali ujenzi wa barabara

WANANCHI wa mtaa wa Chitandi Halmashauri ya Mji Newala mkoani Mtwara wameishukuru serikali kwa kutatua changamoto ya barabara inayojengwa katika mtaa huo kilometa 2 kiwango cha lami iliyogharimu Sh bilioni 1.

Akizungumza Julai 19,2023 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kweynye mtaa huo uliyoandaliwa na mbunge wa Jimbo la Newala Mjini ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum) George Mkuchika, Ofisa Mtendaji wa mtaa huo, Janeth Nyalila amesema mtaa huo ulianzishwa mwaka 1973 hivyo ni miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Hata hivyo una jumla ya wakazi  1,536, kaya 253 ambapo moja ya changamoto iliyokuwa inawakabili wananchi hao ikiwemo barabara hivyo jitihada hizo zilizofanywa na serikali wanafurahia kwasababu sasa wameondokana changamoto hiyo.

Advertisement

Mkazi wa mtaa huo, Ashura Kalole amesema changamoto hiyo ilikuwa inawapa shida kwa kipindi kirefu akina mama hao hasa wakati wa ujauzito wanapotaka kujifungua walikuwa wakibebwa kwenya vitanda  kutoka mtaani hapo kwenda mjini humo kufata huduma ya afya kupitia barabara hiyo yenye mlima mrefuakini sasa wanafurahia kuona barabara inapitika vizuri.

Mkazi wa mtaa huo  Zainabu Saidi ‘’Mtaa wetu ulianza muda mrefu sana nimezaliwa nimeukuta hakukuwa na huduma yoyote ile kama vile barabara lakini leo hii tunaona maendeleo tunayoletewa na serikali yetu, mbunge wetu, diwani kwakweli tunashukuru sana hatuna cha kuwapa zaidi ya shukurani sasa hivi barabara nzuri inapitika.” amesema

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Newala Mhandisi Silvester Balama amesema katika bajeti ya mwaka 2022/23 kupitia mipango ya matengenezo ya kawaida ya barabara na miradi ya maendeleo halmashauri hiyo walitengewa  Sh bilioni 1.5 ambapo walikuwa na ujenzi wa barabara ya Chitandi kilometa mbili na walitengewa Sh bilioni 1 huku gharama ya mkandarasi ikiwa ni Sh milioni 975.

Aidha mpaka sasa  mradi huo umekamilika kwa kilomita 1.6 na kubaki  mita 400 ambazo zinajengwa kwa kiwango cha changarawe na zege na matarajio hadi kufikia Julai mwishoni  mwaka huu mradi huo utakuwa umekamilika ili wananchi waanze kutumia barabara hiyo.
Mwisho.