DAR ES SALAAM: WANANCHI wa hali ya chini katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wamefikiwa baada ya kuanzishwa kwa shule 10 zenye mchepuko wa kiingereza ambazo gharama zake ni nafuu ikilinganishwa na zile za binafsi.
Hayo yameelezwa na Ofisa Elimu ya Awali na Msingi katika halmashauri hiyo, Hossen Mghewa alipozungumza na HabariLeo.
Amezitaja shule hizo kuwa ni Diamond, Olympio, Zanaki, Bunge, Mzizima, Mikongeni, gogo(Chanika), Kisutu, Yangeyange (Msongola) na Majani ya Chai (Kipawa).
“Tumeamua kuwa na shule hizi za mchepuo wa kingereza kwa kuwa nia ya serikali ni kusaidia wananchi wa kipato cha chini.
“Wananchi wanahitaji kuwapeleka watoto shule hizo za mchepuko wa kiingereza lakini wana uwezo mdogo,” amesema.
Kwa maelezo yake shule hizo za mchepuo wa kiingereza zinatozwa Sh 400,000 kwa mwaka tofauti na shule ambazo ni za wawekezaji binafsi.
Amekiri mwitikio wa wanafunzi katika shule hizo ni mkubwa, lakini bado wanaona shule walizonazo ni chache wanahitaji kuziongeza.