Wananchi Iringa wapata ushauri wa kisheria bure

WANANCHI wasio na uwezo wa Manispaa ya Iringa na vitongoji vyake wamejitokeza katika viwanja vya Bustani ya manispaa hiyo kupata msaada wa ushauri wa kisheria unaotolewa bure na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Kanda ya Iringa.

Mawakili wa kujitegemea zaidi ya 50 ambao ni wanachama wa chama hicho watakuwepo katika viwanja hivyo leo na kesho kufikisha huduma hiyo kwa wenye uhitaji.

Mwenyekiti wa kanda hiyo , Moses Ambindwile amesema; “Tunawakaribisha wananchi wote wanaohitaji msaada wa kisheria katika masuala yote ikiwemo mirathi, ndoa, ardhi na biashara.”

Ambindwile alisema ikiwa unastahili msaada wa kisheria, utapewa maelekezo kuhusu hatua inayofuata na usaidizi katika kesi yako au suala la kisheria.

Alisema ndani ya siku mbili, wanatarajia kutoa huduma hiyo kwa wananchi zaidi ya 100 na akawata waendelee kujitokeza.

Mwakilishi wa kampuni ya uwakili ya BLS, Barnabas Nyalusi amesema kampuni yao imedhhamini huduma hiyo ya ushauri wa kisheria ikitambua kwamba mahakama ni msingi muhimu wa mfumo wa kisheria na demokrasia.

Alisema kanda yao ina imani kubwa na mahakama na namna inavyofanya kazi bila kuingiliwa na mamlaka nyingine, ikiwa ni pamoja na serikali na hiyo ni muhimu kwa kutoa haki na kudumisha usawa na utawala wa sheria katika jamii.

Nyalusi alisema Uhuru wa mahakama unahakikisha kuwa kila raia anaweza kutafuta haki zake kwa imani katika mfumo wa kisheria.

“Kwahiyo tupo hapa katika viwanja hivi tunawasubiri wasio wenye uwezo na wanaohitaji msaada wa kisheria waje na changamoto zao za kisheria tuwasaidie kwa kuwapa msaada wa ushauri wa kisheria,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button