WANANCHI 157,110 kutoka halmashauri za wilaya 42 ya mikoa tisa ya Kanda ya Kaskazini Mashariki wanatarajia kunufaika na huduma za afya, ulinzi na usalama wa mtoto na uanzishwaji wa vikundi vya kuweka na kukopa kupitia mradi unaofadhiliwa na Shirika la Kimaendeleo la Kimarekani (USAID).
Mradi huo wa miaka mitano wa USAID – Kizazi Hodari umeanza mwaka wa fedha 2023/2024 na unatekelezwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Makao makuu Arusha.
Ofisa Mwandamizi, Ustawi, Mashauri, Jinsia, Ulinzi wa Usalama wa mtoto, Emmanuel Sule alisema hayo katika banda la mradi huo viwanja vya shule ya sekondari Morogoro kwenye maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani kitaifa , Disemba mosi mwaka huu.
Sule alisema Kanisa la KKKT mbali na kujihusisha na huduma za kiroho pia linatoa huduma za kijamii kumhudumia mwananchi kupitia kurugenzi ya afya, Idara ya afya inayofanya kazi kupitia hospitali .
Alisema kwa sasa kanisa hilo linatekeleza mradi wa Kizazi Hodari unalenga kuimarisha afya , ustawi, ulinzi na usalama wa watoto kupitia mipango ambayo mradi unaitekeleza.
Sule alisema tayari umeweza kuzifikia kaya 67,337 sawa na asilimia 103 katika huduma mbalimbali za kiafya, ulinzi na usalama wa mtoto huduma za vikundi vya kuweka na kukopa na kwamba walezi wa watoto waliolengwa wametambuliwa na kuhudumiwa katika maeneo mbalimbali za mradi .
Hivyo alitoa wito kwa walengwa hasa katika kipindi cha kumbukizi ya maadhimisho ya wiki ya ukimwi duniani, jamii yote kwa ujumla iendendelee kushirikiana katika kuhakikisha maambukizi mapya hayatokei .
Kwa upande wake Ofisa Mashauri Ulinzi na Usalama wa Mtoto na Maswala ya Jinsia wa kanisa la KKKT, Mwajuma Karisha alisema , mradi huo hautoi huduma kwa mlengwa moja kwa moja, bali ni kwa kutumia huduma unganishi.
Karisha alisema huduma hizo zina waunganisha walengwa wa mradi na watoa huduma mbalimbali ambao ni wadau wa maendeleo nchini hususan katika maeneo yanayozunguka mradi huo.
Alitolea mfano vikundi vya hazina yetu ambavyo vimepewa elimu mbalimbali na kuviunganisha na wadau zikiwemo taasisi za kifedha , wadau wa maendeleo , maofisa ugani ,na mpango wa asilimia 10 zinazotokana na halmashauri ili kupata fursa za mikopo.
Karisha alisema, vikundi hivyo vinanufaika na fursa nyingine vikiwemo vya vijan kupatiwa elimu ya mafunzo ya stadi na ufundi katika chini ya Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA).
“ Mfano kikundi hiki cha vijana cha RICH BEFORE 40 kimeanzisha biashara zao za ujasiriamali na huu ni mfano tuu wa zaidi ya vikundi vinne ambavyo vinahudumiwa na mradi huu kwa vijana na wanawake “alisema Karisha
Alisema mradi unawaunganisha pia wanawake na fursa za kilimo kwa kuwatumia maofisa ugani wa serikali na maofisa maendeleo ya jamaii na wadau wengine wa kilimo ili waweze kupatiwa misaada ya mbegu , mitaji , elimu ya kilimo bora ya kujiendesha kwenye miradi midogo ya vikundi vyao.