Wananchi Katavi waishukuru Serikali huduma ya afya

Wananchi wa Kata ya Kazima Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi wameishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma ya afya kwa kuwajengea kituo cha afya jirani.

Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf aliyefika kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa katika Kata hiyo wamesema awali walilazimika kutembea umbali mrefu hadi Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi au kituo cha afya Town clinic ili kupata huduma ya matibabu.

Advertisement

“Uwepo wa kituo hiki kitawahudumia hata baadhi ya wananchi wa Kata jirani kwa mfano Kata ya Kasokola ambayo bado haina kituo cha afya” amesema ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Lusubilo Mwakabage

Aidha Mkuu wa Wilaya Jamila Yusuf ametoa shukrani zake kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Wilaya hiyo shilingi Bilioni 1.25 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya afya.

Vilevile ameupongeza uongozi wa Kata hiyo kwa namna wanavyo simamia ujenzi wa kituo hicho huku akiwataka kuongeza umakini wa usimamizi hasa wa wizi wa vifaa na kumuagiza Mkurugenzi kuhakikisha ifikapo januari mosi, 2023 kituo hicho kuanza kutoa huduma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbuli amesema kituo hicho kinajengwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza walipokea shilingi milioni 250 kwa maelekezo ya kukamilisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na maabara pamoja na kichomea taka.

Kumbuli amesema Kituo hicho kinachojengwa kwa fedha zitokanazo na tozo za miamala ya simu kinatarajia kukamilika Desemba 20 mwaka huu na kitawanufaisha wananchi wapatao 20,000 wa Kata hiyo