Wananchi kupata taarifa OCRI wakiwa nyumbani

KUTOKANA na kuzinduliwa kwa kituo cha Huduma kwa wateja katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (OCRI), wananchi sasa watapata elimu na taarifa za ndugu zao wagonjwa kwa haraka kupitia huduma hiyo.Mpango huo wa kituo cha huduma kwa wateja umewezeshwa na benki ya CRDB kupitia mpango wake wa CRDB benki Marathon.

Akizungunza leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Saratani Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, aliwataka wananchi kuchukua hatua za mapema kupima ugonjwa wa saratani, kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kufanya mazoezi.

Pia amewaomba wataalamu wa afya nchini, kuendelea kutoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa wa saratani.

“Tujitokeze kwa wingi kupima saratani na wanaume kupima saratani ya tezi dume, kupima mapema inakusaidia kupata matibabu, kupona na kuendelea na maisha, lakini la pili tufanye mazoezi,”amesema.

Pia Makala, ameishukuru Benki ya CRDB kwa kujenga kituo cha mawasiliano na huduma kwa wateja katika taasisi hiyo.

 

“Namshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa maboresho makubwa anayoyafanya katika sekta ya afya nchini, ikiwemo ORCI.

Makala ameitaka taasisi ya ORCI kukitunza kituo hicho,kidumu kiendelee kuwahudumia wananchi,” amesema.

Amewashukuru watoa huduma na madaktari wa ORCI, kwa huduma nzuri wanazotoa kwa Watanzania .

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB , Abdulmajidy Nsekela, amesema benki hiyo imefanikisha kujenga kituo cha huduma kwa wateja katika taasisi ya ORCI, ambacho kitasaidia wananchi kupiga simu moja kwa moja hosptalini hapo na kupatiwa huduma.

Amesema kituo hicho kitakuwa chachu ya kuboresha huduma katika taasisi ya ORCI.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ORCI, Dk Julius Mwaisalage,alisema taasisi hiyo inatoa huduma za kinga,chanjo ya kujikinga na homa ya ini na kufanya uchunguzi wa awali wa ugonjwa wa saratani.

Habari Zifananazo

Back to top button