Wananchi kupimwa bure magonjwa ya moyo
DSM; Kuelekea Maadhimisho ya siku ya Moyo Duniani Septemba 29 kila mwaka, Chama cha Madaktari Bingwa wa Moyo Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wanatarajia kutoa huduma za upimaji bure katika Tawi la JKCI, hospitali ya Dar Group iliyopo jijini Dar es Salaam.
Takwimu zinaonesha takribani watu milioni 20 hupoteza maisha duniani kutokana na magonjwa ya moyo, ambapo pia hapa nchini takribani asilimia 13 hupoteza maisha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Moyo Tanzania( TCS), Dk Robert Mvungi amesema kambi maalum ya matibabu itakayohusisha uchunguzi na utambulishi wa kujua viashiria ya magonjwa ya moyo itafanyika kwa siku mbili Septemba 29 na 30,2023.
“Nchi yetu imepiga hatua sana katika matibabu ya moyo na chama kimeona ni heri kushirikiana na wadau wakubwa ambao wamehusika kubadilisha hadhi ya Tanzania katika kutibu na kukinga magonjwa ya moyo,”ameeleza.
Amesema kutakuwa na matembezi ambayo yataanza saa 12:00 asubuhi Septemba 30 mwaka huu.
“Tutafanya uchunguzi wa afya Dar Group Hospital, watu wote wanakaribishwa kuangalia na kutambua afya yao na tuna matembezi maalum tutatembea kutoka Uwanja wa Uhuru Chang’ombe Temeke hadi Tazara pale Dar Group.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amesema kwa kushirikiana na chama kwa pamoja wanaadhimisha Siku ya Moyo Duniani, ambapo watapima wagonjwa matatizo ya moyo na kuwaomba wananchi wajitokeze.