Wananchi kupimwa kubaini magonjwa yasiyoambukiza

WIZARA ya Afya imesema inakusudia kuwa na utaratibu wa kuwapima wananchi wanaokwenda kupata huduma za afya ili kujua endapo wana magonjwa yasiyoambukiza.

Mratibu wa Kinga na Magonjwa Yasiyoambukiza katika Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza, Goodluck Tumaini, alisema hayo Jumatano Dar es Salaam wakati wa kikao na wahariri wa vyombo vya habari kujadili kukabiliana na magonjwa hayo.

Tumaini alisema wanakusudia kuwapima watu wanaokwenda kupata huduma za mama na mtoto pamoja na wanaoishi na virusi vya Ukimwi ili kujua endapo wana magonjwa yasiyoambukiza.

Alisema wizara imeimarisha huduma muhimu katika vituo vya afya na kwa watoa huduma, hivyo ni rahisi kuwapima watu wanaokwenda kupata huduma, ili kujua hali zao na kusaidia katika kukabili magonjwa hayo.

Aliwaomba wahariri na waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na serikali  kuelimisha jamii kuhusu magonjwa hayo yanayoigharimu serikali fedha nyingi.

Mwenyekiti wa Chama cha Kisukari Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Profesa Andrew Swai alisema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakiongezeka nchini ikilinganishwa na miaka ya 1980.

Profesa Swai alisema asilimia 33 ya vifo vya Watanzania vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza na wengi wanakufa kabla ya kutimiza umri wa miaka 70.

Magonjwa yasiyoambukiza ni magonjwa yasiyo na vimelea vinavyoweza kusambazwa. Mfano, ni magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kisukari, kuoza meno, magonjwa ya akili na mengine ya kurithi kama vile ugonjwa wa selimundu.

Magonjwa hayo yanaongezeka kwa kasi na kuathiri hata watu wenye umri mdogo wakiwamo watoto.

Kwa mujibu wa Profesa Swai, sababu za kuongezeka kwa magonjwa hayo ni mabadiliko ya mtindo wa maisha ikiwamo kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa, matumizi ya pombe, tumbaku na dawa za kulevya, utawala duni wa msongo wa mawazo na kutopata usingizi wa kutosha.

Tumaini alieleza kuwa serikali imechukua hatua kuzuia na kukabiliana na magonjwa hayo ikiwamo kutoa elimu kwa kuja na mikakati na miongozo  ukiwamo Mwongozo wa Kuushughulisha Mwili dhidi ya Tabiabwete Tanzania wa mwaka 2022.

Mwongozo huo unakusudia kutoa mapendekezo ya kiafya kwa watoto na vijana, watu wazima na wazee juu ya kiasi cha kushughulisha mwili kuleta faida za kiafya.

 

Habari Zifananazo

Back to top button