Wananchi Majalila wasaidia ujenzi kituo cha Polisi

WANANCHI wa Kijiji cha Majalila, Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, wameungana na serikali kujenga kituo cha Polisi kwa kuchangia fedha na nguvu kazi.

Akipokea mifuko 50 ya saruji yenye thamani ya Sh milioni moja, kutoka kwa Mbunge wa Jimbo Mpanda Vijijini, Seleman Kakoso, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, amemuagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi kuhakikisha wanasimamia michango hiyo kusiwepo upotevu wa aina yoyote.

Buswelu ametoa shukrani kwa wananchi na wadau mbalimbali, waliojitokeza kuchangia ujenzi wa kituo hicho.

“Serikali ya wilaya pamoja na wananchi wote na nguvu ya Mbunge Kakoso, wameamua kushirikiana kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga kituo cha Polisi cha kisasa, nawashukuru sana,” alisema Buswelu.

Awali akikabidhi mifuko hiyo kwa niaba ya Mbunge, Katibu wa Mbunge, Said Wambali amesema ofisi ya mbunge imeona iungane na wananchi pamoja na wadau kuunga juhudi za serikali kujenga kituo hicho, ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi kituo hicho, Ramadhan Nyembe amemhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa michango iliyotolewa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali, haitapotea na atahakikisha inasimamiwa kikamilifu.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Majalila wamesema kukamilika kwa kituo hicho kutawasaidia kuishi kwa amani, kwa kuwa wanaamini uhalifu utadhibitiwa na itawarahisishia kufikika kwa haraka kituoni hapo, kwani kwa sasa wanafuata huduma Kijiji cha Kibo, ambapo ni umbali wa kilomita takriban 10 kutoka kijijini hapo.

Hadi sasa ujenzi upo hatua ya msingi, ambapo wananchi wamekuwa wakichangia fedha taslimu, mifuko ya saruji, nondo pamoja na nguvu kazi ikiwa ni pamoja na kuchimba msingi wa ujenzi wa kituo hicho.

Habari Zifananazo

Back to top button